Yanga mambo ni moto! Ni baada ya viongozi wa timu hiyo kuanza mchakato mpya wa kuwalipa wachezaji wake posho kwa wiki ambayo ni Shilingi 100,000.
Hiyo ni Hela ya mboga tu ya kujikimu haihusiani na ushindi wala mechi. Awali, hawakuwa wanalipwa hivyo kabla ya uongozi mpya wa timu hiyo kuingia madarakani na kuanza mchakato huo wa kuwalipa wachezaji wake posho hizo ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwapoka ubingwa Simba. Kwenye msimu uliopita na huu wa Ligi Kuu Bara, Simba inayoongozwa na staa wake Mnyarwanda, Meddie Kagere walikuwa wanalipwa posho ya Shilingi 400, 000 kwa kila wanapopata ushindi. Lakini kwa sasa Yanga, kila wiki mshambuliaji wa timu hiyo Mkongomani, David Falcao Molinga na wenzie wana uhakika wa kuvuta Shilingi 100, 000 huku akisubniria bonasi ya ushindi itakayotolewa na wadhamini wao GSM ambao wameahidi kutoa Sh Mil. 10 kwa kila watakapopata ushindi. “Uongozi unajaribu kufanya kila jitihada za kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri ya ushindi na ndiyo sababu ya kuwapatia posho ya Sh 100, 000 kila wiki bila ya kujali anacheza au anakaa benchi,”kilisema chanzo chetu cha kuaminika. “Katika kuhakikisha wachezaji wetu wanacheza kwa kujitoa katika timu, tumewalipa mishahara yao ya miezi miwili(juzi Jumatatu), hivyo hakuna mshahara tunaodaiwa,”alisema mtoa taarifa huyo.
0 Comments