Nahodha wa Arsenal Granit Xhaka amekiri kuwa “waliwaogopa sana” Watford katika mchezo ambao uliisha kwa sare ya 2-2. Pierre-Emerick Aubameyang alitikisa nyavu mara mbili katika kipindi cha kwanza, na ikaonekana kama Arsenal tayari imekwisha umaliza mchezo huo.
Kipindi cha pili hata hivyo Watford ambao walikuwa ugenini walirudi kwa kasi na kusawazisha kupitia Tom Cleverley na penati ya dakika za lala salama iliyopigwa na Roberto Pereyra.
Watford ilikamilisha mchezo huo ikipiga mashuti 31, 23 kayi ya hayo wakipiga kipindi cha pili.
“Hakuna mtu ambaye alikuwa akiutaka mpira. Mwishowe tunafuraha kupata walau alama moja,” Xhaka amesema.
“Hatukuonesha kiwango chetu kipindi cha pili, tulikuwa na woga wa kupitiliza.”
Goli la kwanza la Watford lilipatikana baada ya mlinzi wa Arsenal Sokratis Papastathopoulos kupoteza mpira katika eneo la hatari na kumfanyia wepesi Cleverley kuwaadhibu.
Toka kuanza kwa msimu uliopita, wachezaji wa Arsenal wamefanya makosa 14 kwa ujumla ambayo yamepelekea wapinzani kuwaadhibu katika ligi ya Premia – ambayo ni wastani wa makosa mawili zaidi ya klabu nyengine yeyote.
Mashuti 31 ambayo Watford iliyapiga ni mengi zaidi ambayo Arsenal walikutana nayo katika mechi ya Primia toka kampuni ya Opta ilipoanza kukusanya takwimu za mechi 2003-04.
“Kila timu ya ligi ya Primia ni ngumu na inaweza kushinda. Inabidi uwe umetulia, uoneshe mchezo mzuri na ukomavu wa kiakili. Hatukuwa hivyo kwenye mchezo huu, ” Xhaka ameongeza.
Baada ya kuanza kwa ushindi wa mechi mbili dhidi ya Newcastle na Burnley, Arsenal sasa wamecheza michezo mitatu bila ya kuambulia ushindi. Walifungwa na Liverpool kisha wakatoka sare na Tottenham na sasa Watford.
0 Comments