Klabu ya Yanga imeendeleza ubabe wake ligi kuu baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate mchezo uliopigwa dimba la CCM Kilumba jijini Mwanza.
Joseph Guede ndiye aliyekuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Singida Fountain Gate baada ya kutoa krosi iliyomgonga beki wa Singida Fountain Gate na kumfanya kipa Benedikt Haule ashindwe kuokoa mpira uliopita moja kwa moja nyavuni.Bao la pili liliwekwa kimiani kwa shuti kali la Aziz Ki aliyepokea pasi kutoka kwa Clement Mzize na bao la tatu lilifungwa na Guede kwa kichwa kilichomshinda golikipa Benedikti Haule
Kwa matokeo haya klabu ya Yanga imeendelea kusalia kileleni ikifikisha alama 55 kwenye michezo 21 waliyocheza na nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam FC wenye alama 50 baada ya michezo 22 huku nafasi ya 3 ikishikiliwa na Simba wenye alama 46 baada ya kucheza michezo 20.
Matokeo haya ni salamu kuelekea mchezo muhimu wa ligi kuu tarehe 20 April dhidi ya Simba ambao katika michezo minne mfululizo ya mashindano mbalimbali wameambulia sare 1 na kupoteza michezo mitatu.
Simba waliondoshwa michuano ya ligi ya mabingwa Afrika baada ya kukubali kipigo cha jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Al Ahly na baadaye walitolewa michuano ya CRDB Federation Cup dhidi ya mashujaa na kisha kupata sare ya bao1-1 dhidi ya Ihefu mchezo wa ligi kuu.
kwa upande wa Yanga wao walipata sare michezo miwili ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns na kuondoshwa kwa mikwaju ya penati lakini walifanikiwa kuingia hatua ya 8 michuano ya CRDB federation Cup baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
0 Comments