advertise with us

ADVERTISE HERE

MAKALA:TAIFA STARS WAPITE NJIA WALIZOPITA DR CONGO AFCONN.

 Anaandika mchambuzi nguli Maggid Mjengwa

Tafakuri Jadidi:

Adili Ya Kisa Cha Mobutu Na Wajukuu Zake…

Mwaka huu inatimu Nusu Karne, naam, miaka 50 tangu Mobutu wa Zaire, mwaka ule wa 1974 alipotuma kikosi chake Ujerumani kilichojaa wachawi pia.

Ni kwenye Kombe la Dunia. Zaire, ambayo sasa inaitwa DR-Congo, ilifanya madudu.

Jana usiku tumewaona ‘ Wajukuu’ wale wa Mobutu wakifanya makubwa Afcon. Nawaona wakitinga Fainali, hawataishia nusu.

Swali:

Tunajifunza nini kutoka kwa ‘ Wajukuu wale wa Mobutu’?

Jibu:

Nilipata kuuliza hili majuzi tu. Kwamba sisi Tanzania tunayo safari lakini si ndefu sana kufikia mafanikio ya kwenda Afcon kushindana kufika robo hata fainali ya Afcon na si kupigania tu tusitolewe kwenye hatua ya makundi.

Ni kwa hatua za kufanya maamuzi magumu kama yanayofanywa na nchi kwa sasa, mathalan, kuwapa fursa Watanzania Diaspora na hata ya kuwapa ‘ Uraia Pacha’  wenye nasaba na Tanzania waliozaliwa nje ya nchi lakini wameonyesha kuwa na vipaji na uwezo wa kucheza soka. Afrika Wahenga walisema, usijali paka ni wa rangi gani, ilimradi ni wa nyumbani kwako na anakukamatia panya.

Tunajua, mwanzo  ni mgumu. Ni kweli, baadhi yao waliopewa fursa ya kujiunga na Stars hawakuonyesha uwezo mkubwa, lakini, ndio mwanzo wa vipaji vingine kuonekana na hata kuendelea na kazi ya ku- skauti huko waliko na kuwakusanya.

Tukipata idadi ya kutosha ya vijana chini ya miaka 18 waliokulia kwenye akademi za wenzetu walioendelea, kisha tukawapa fursa, basi, miaka si mingi nasi tutakuwa kwenye kiwango cha kuwania kufika fainali na kuchukua ubingwa iwe kwenye Afcon na mashindano mengine.

Ona DR- Congo walikotoka…

Kwa kuanzia, ukiona vikosi vya timu za vilabu kule Ufarasana na Ubelgiji, hukosi kuwakuta ‘ Wajukuu wa Mobutu’ kwa maana ya wachezaji wenye asili ya DR- Congo.

Kikosi cha DR- Congo kinachoshiriki Afcon inayoendelea  kina wengi waliozaliwa ama Ubelgiji au Ufaransa. Na wanachezaji wa vilabu vyenye majina Ufaransa, Ubelgiji na kwengineko duniani. Ni  kuanzia golikipa wao Lionel Mpasi mpaka mshambuliaju Yoane Wissa.  Bado una kina Mmbemba, Kakuta Mambenga, Yannick Balasie, Theo Bongouda ,  Diangana na Kayembe.

Mle uwanjani jana ni Mayele tu ndiye jina ambalo Watanzania tulilolizoea na tumemwona akicheza ‘ Kwa Mkapa’ mara kwa mara. Wanaye pia Inonga.

Si ndio, hata kule Ubelgiji tumewaona  ‘ Wajukuu wa Mobutu Sese Seko Kuku Mbangu wa Zabanga.’ Wachezaji aina ya Lukaku na wenzake. Wana asili ya Zaire ya Mobutu na sasa wanaichezea Ubelgiji.

Wazazi wao ni wa kutoka DR Congo. 'Babu' yao Mobutu mwaka 1974 alikodi ndege nzima kuwabeba wachawi kwenda kuwasaidia ' The Leopards'- chui wa Mobutu. 

Zaire mwaka 1974 ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiafrika  Kusini ya Jangwa la Sahara kucheza kombe la dunia. 

Kwenye kikosi cha Zaire 1974 kulikuwa na akina Boba Lobilo, huyu alikuwa beki makini kama Kompany, alikuwapo pia Mwepu Ilunga na wengine.

Wakongo wa sasa wameshatoka huko kwenye kuamini ‘ Ndumba na ngae’ ili wafanikiwe. Wako Kisayansi na kiufundi zaidi. 

Tunakokwenda sisi?

Kuna mwanga. Maana tumeshakubali kubadilika.Post a Comment

0 Comments