Baada ya mabosi wa timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kuzidi kuwa ‘siriaz’ na ishu ya kuipata saini ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, uongozi wa Simba unatarajiwa kukaa chini kujadili ofa ya mchezaji huyo pamoja na ofa za wachezaji wengine.
Manula amekuwa kwenye kiwango msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amecheza jumla ya mechi tano kwenye hatua za makundi na kukusanya clean sheet tatu na ameokota nyavuni mabao mawili.
Timu yake pia imetinga hatua ya robo fainali jambo ambalo limezifanya timu nyingi Afrika ikiwa ni pamoja na Al Merrikh ya Sudan nayo kuipigia hesabu saini ya Manula ambaye ni mzawa.
Habari kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya Simba zimeeleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba itakaa kujadili ofa za wachezaji wao huku kipaumbele ikiwa ni Manula.
“Mamelodi Sundowns pamoja na timu nyingine zimeonekana kuwa hazitanii kwa kuleta ofa ambapo tayari bodi ya Simba inatarajiwa kukaa kujadili suala la wachezaji wao ambao wanahitajika na timu nyingine.
"Kutokana na ofa ilivyo inaonekana kwamba mambo yatakwenda vizuri hivyo baada ya kikao itajulikana hatma ya Manula ndani ya Simba pamoja na wachezaji wengine,” alisema mtoa taarifa huyo aliyeomba hifadhi ya jina.
Mamelodi Sundowns inahitaji mbadala wa Denis Onyango raia wa Uganda ambaye alisema kuwa ana mpango wa kustaafu huku dau ambalo wamemuwekea Manula linatajwa kuwa shilingi milioni 500 ili kupata saini yake.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, hivi karibuni alisema kuwa ikiwa watapokea ofa kutoka timu inayohitaji mchezaji wa timu hiyo hawataweza kukataa ikiwa itawafaa na mchezaji mwenyewe akakubali kuondoka.
0 Comments