Klabu ya Yanga imemrejesha nyumbani beki wa wake kati Abdallah Shaibu maarufu kwa jina la Ninja huku akipewa mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo mpaka mwaka 2022. Awali Ninja alipata dili la kucheza nje ya nchi lakini mambo hayakumwendea sawa.
Ninja alipata timu nchini Serbia iliyokuwa inaitwa MFK Vyskov iliyomtoa kwa mkopo akacheze ndani ya Klabu ya LA Galaxy nchini Marekani.Baadaye alirudi tena kwenye Klabu yake ya MFK Vyskov ambako alikosa nafasi ya kudumu kikosi cha kwanza jambo lililomfanya arejee nyumbani Tanzania.
Alianza majaribio ndani ya Yanga chini ya Luc Eymael aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga ambaye amefutwa kazi Julai 27 na hatimaye ametambulishwa rasmi kurejea kwenye timu yake ya zamani.
Huu unakuwa ni usajili wa tano kwa Yanga ambayo ipo kwenye mchakato wa kuboresha kikosi ikiwa imemalizana na Bakari Mwamnyeto ambaye ni beki kutoka Coastal Union, Zawadi Mauya kiungo kutoka Kagera Sugar, Yasin Mustapha beki kutoka Polisi Tanzania na Wazir Jr mshambuliaji kutoka Mbao FC.
Usajili wa mchezaji huyo umeibua shangwe kwa mashabiki wa Yanga kwani alikuwa kwenye kiwango kizuri kwenye msimamo wa 2017/18 kabla ya kutimka nchini.Baadhi ya mashabiki wameupongeza usajili huo wakiuita ni usajili wa kimkakati kwani Ninja ni Yanga damu na uwezo wake unafahamika.
0 Comments