MOLINGA BABA LAO AWAPELEKA YANGA NUSU FAINALI FA


Yanga SC wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba usiku huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lakini haukuwa ushindi mwepesi kwa wana Jangwani hao, kwani walilazimika kutoka nyuma baada ya Kagera Sugar inayofundishwa na kocha mzalendo, Mecky Mexime kutangulia kwa bao la kiungo wake Awesu Awesu.


Awesu alimtungua kipa Metacha Boniphace Mnata dakika ya 20 kwa shuti la kiufundi la umbali wa mita 20 baada ya kupokea pasi ya kisigino ya kiungo mwenzake, Yusuph Mhilu, mchezaji wa zamani wa Yanga.


Mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga akaisawazishia Yanga SC kwa kichwa dakika ya 52 akimalizia pasi ya kichwa ya kiungo Mrisho Khalfan Ngassa, mchezaji wa zamani wa Kagera Sugar.

Kiungo Deus David Kaseke akaifungia Yanga bao la ushindi dakika ya 76 kwa penalti iliyotolewa na refa Shomar Lawi wa Kigoma baada ya Ngassa kuangushwa na Nyosso. Ilionekana Ngassa amekatiwa nje ya mstari, lakini akaangukia ndani.


Dakika mbili baadaye Awesu akatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumtolea maneno machafu refa. Molinga akashindwa kuendelea na mchezo dakika ya 83 baada ya kuumia kufuatia kugongana na Nyoyo na nafasi yake kuchukuliwa na Tarik Seif Kiakala.


Mechi iliyotangulia Namungo FC ilikuwa ya kwanza kutinga Nusu Fainali baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Alliance FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, mabao ya Bigirimana Blaise kwa penalti dakika ya 41 na George Makang’a dakika ya 84.


Sasa Namungo FC itamenyana na mshindi kati ya Sahare All Stars na Ndanda zinazomenyana kesho jioni Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Yanga itamenyana na mshindi kati ya Azam FC na Simba SC zinazomenyana kesho Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam usiku. 


Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Haruna Niyonzima/Patrick Sibomana dk84, David Molinga/Tarik Seif dk84, Ditram Nchimbi/Mrisho Ngassa dk46 na Deus Kaseke/Kelvin Yondan dk90+3.


Kagera Sugar; Said Kipao, Mwaita G
ereza, David Luhende, Hassan Isihaka, Juma Nyoso, Zawadi Mauya, Yusuph Mhilu/Nassor Kapama dk, Abdallah Seseme, Kelvin Sabato/Erick Mwaijage, Ally Ramadhan ‘Kagawa’/Peter Mwalyanzi na Awesu Awesu.

Post a Comment

0 Comments