MBEYA CITY YAIADHIBU COASTAL UNION
Mbeya City imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Kwa ushindi huo, Mbeya City inayofundishwa na kocha Amri Said ‘Stam’ inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 33, ingawa inabaki nafasi ya 18 ikizidiwa wastani wa mabao na Ndanda SC ya Mtwara iliyo nafasi ya 17.


Coastal Union inabaki nafasi ya tano na pointi zake 48 baada ya kucheza mechi 33 pia wakiendelea kuizidi wastani wa mabao tu Polisi Tanzania inayofuatia nafasi ya sita.


Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Isihaka Mwalile aliyesaidiwa na Abdul Malimba wote wa Dar es Salaam na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko tayari Mbeya City walikuwa mbele kwa mabao 2-0. 

Mabao hayo yalifungwa na Abasarim Chidiebere dakika ya tisa akimalizia kazi nzuri ya Abdul Suleiman na Rehani Kibingu dakika ya 35 akimalizia pasi ya Peter Mapunda.

Kipindi cha pili Coastal Union iliyo chini ya kocha Juma Mgunda ilikianza vyema na kufanikiwa kupata bao dakika ya 69 kupitia kwa Ibrahim Ame kabla ya Peter Mapunda kumalizia pasi ya Patson Shigala kuifungia Mbeya City bao la tatu dakika ya 87.

Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Haroun Mandanda, Baraka Mtafya, Hassan Mwasapili, Ibrahim Ndunguli, Rolland Msonjo, Emmanuel Memba, Rehani Kibingu/Daniel Lukandamila dk89, Abdul Suleiman, Abasarim Chidiebere/Patson Shigala dk83, Peter Mapunda na Suleiman Ibrahim.

Coastal Union; Soud Abdallah ‘Dondola’, Ayoub Masoud/Hassan Kibailo dk46, Hance Masoud, Ibrahim Ame, Bakari Mwamnyeto, Salum Ally, Hassan Ally/Mudathiri Said dk46, Ayoub Semtawa, Hamisi Kanduru, Ayoub Lyanga/Shaaban Iddi dk59 na Issa Abushehe/Hamad Majimengi dk78.

Post a Comment

0 Comments