Kinyang'anyiro cha Kombe la mataifa bingwa Afrika kilichotarajiwa kufanyika mwaka ujao 2021 kimeahirishwa hadi Januari 2022 na shirikisho la kandanda barani Afrika (Caf) kutokana na mlipuko wa virusi vya corona huku shindano kama hilo upande wa wanawake likifutiliwa mbali.
Shindano la wanaume lilitarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka ujao.Katika habari nyingine, kinyang'anyiro cha kombe hilo miongoni mwa wachezaji wanaocheza barani Afrika CHAN ambalo lingechezwa mwezi Aprili sasa litafanyika Januari 2021.Mashindano yote mawili yanatarajiwa kufanyika nchini Cameroon.
''Afya ndio kitu muhimu kwetu lazima tuwe macho'', rais wa Caf Ahmad Ahmad alisema katika mkutano na vyombo vya habari akitangaza uamuzi huo.
Hatua hiyo ina maana ya kwamba michuano hiyo inayofanyika mara mbili kwa mwaka sasa itafanyika mwaka mmoja na kombe la dunia la 2022 - kitu kilichofanyika mara ya mwisho mwaka 2010.
Michuano hiyo ilifanyika mwaka 2013 - huku mashindano ya mwaka huo yakifanyika mwaka mmoja baada ya mwaka huo ili kuzuia kuwa katika mwaka mmoja na kombe la dunia, uamuzi ambao ulihatarisha kuyapatia fursa mataifa ya Afrika katika kombe la dunia kwa kuyaongezea msimu wa mashindano.
Huku michuano hiyo ikitarajiwa kufanyika Januari kama ilivyo kawaida, mashindano ya hivi karibuni ya komba la Afcon 2019 yalihamishwa na kufanyika katika msimu wa joto katika juhudi za kuzuia kuingiliana na mashindano ya ligi za bara Ulaya.
Hatua hii pia ilitarajiwa kuathiri kombe hilo la Cameroon, lakini ikabadilishwa hadi Januari kutokana na hali ya hewa nchini humo mbali na uwezekano wa kuingiliana na michuano ya kombe la dunia.
Uamuzi huo una maana kwamba mabingwa wa kombe la klabu bingwa Ulaya Liverpool watacheza msimu wote ujao bila kuwapoteza washambuliaji wao hatari Sadio Mane na Mohamed Salah katika mechi za kimataifa.
Wakati huohuo kufutiliwa mbali kwa kombe la michuano ya mataifa bingwa Afrika miongoni mwa wanawake kumeshangaza wengi wakati ambapo kinyanganyiro hicho kilikuwa hakina mwandalizi.
Mashindano ya wanawake hatahivyo yalipigwa jeki kutokana na uzinduzi mpya wa kombe la mabingwa Afrika 2021 miongoni mwa wanawake.
0 Comments