Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, ametaja sifa mbili alizonazo kiungo Ally Niyonzima zilizomshawishi yeye kumpa mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Niyonzima hivi karibuni alikiri kuwepo kwenye mazungumzo mazuri na Yanga chini ya GSM inayosimamia usajili wake katika kuelekea msimu ujao unaotarajiwa kuwa mgumu.
Wachezaji wengine wanaotajwa kuwaniwa na Yanga ni Michael Saprong (huru), Tuisila Kisinda (AS Vita), Heritier Makambo (Horoya AC) na Bakari Mwamnyeto (Coastal Union).
Eymael amesema kuwa sifa ya kwanza aliyonayo kiungo huyo ni uwezo wake wa kucheza nafasi ya beki wa kati namba 4 na 5.
Eymael aliitaja sifa nyingine ni uwezo wake wa kunyang’anya mipira na kuchezesha timu wakati akiwa na mpira, hivyo hajutii maamuzi yake ya kupendekeza usajili wa kiungo huyo mwenye faida kubwa katika timu.
Aliongeza kuwa tayari amekabidhi orodha ya majina ya wachezaji ambao amewapendekeza walio nao kwenye mazungumzo ili kuhakikisha wanakisuka kikosi imara kitakacholeta ushindani msimu ujao.
“Nimepanga kufanya usajili wa kisasa kabisa utakaoendana na hadhi ya timu yetu na kikubwa kuwapata wachezaji wote muhimu ninaowataka ili kutengeneza kikosi cha ushindani.
“Mengi nimeyapanga katika msimu ujao, kwa kuanza nimepanga kutengeneza kikosi imara kitakacholeta ushindani mkubwa, tayari tupo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa Niyonzima.
“Niyonzima ni kati ya usajili bora kabisa nilioupendekeza katika timu yangu, kwangu ni kiungo bora ambaye huduma yake ninaihitaji katika timu yangu na kikubwa kuiboresha safu ya kiungo ya ukabaji,” alisema Eymael.
0 Comments