Kiungo mshambuliaji wa Simba Luis Miquissone tayari amerejea nchini kuungana na kikosi cha mabingwa hao wa nchi kuanza maandalizi ya ngwe ya lala salama ligi kuu ya Vodacom
Miquissone ametua wakati mwafaka wakati Simba ikitarajiwa kuanza mazoezi ya timu kesho Jumatano
Kurejea kwa Miquissone kunafanya idadi ya nyota wa kigeni ambao bado hawajarejea kuwa wanne ambao ni Meddie Kagere, Clatous Chama, Francis Kahata na Sharaff Shiboub
Katika hatua nyingine, Daktari wa Simba Dk Yassin Gembe amesema wachezaji wote wa timu hiyo wako tayari kurejea uwanjani siku ya Jumatano
Dk Gembe amesema nyota wote watafanyiwa vipimo kabla ya kuanza mazoezi ili kuhakikisha wana afya nzuri
"Baada ya wachezaji kurejea mazoezini watapimwa kuangalia hali zao za kiafya ili kujiridhisha tena kama kipindi walichokuwa mapumziko hawajapata madhara yoyote.
"Nimewasiliana nao wote wako vizuri na wanaendelea na mazoezi binafsi huko walipo kulingana na programu tulizowapa, wakirudi tena tutawapima kujua hali zao katika muda waliokuwa mapumzikoni," Dk Gembe amenukuliwa na tovuti ya Simba
0 Comments