Namungo FC itaikaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utaikutanisha miamba hii inayotesa ndani ya tano bora na shughuli itakuwa pevu kutokana na ubora wa timu zote mbili.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Namungo kumenyana na Yanga tangu ilipopanda ligi msimu huu imecheza mechi 27 na kujikusanyia pointi 49 ikiwa nafasi ya nne huku Yanga ikiwa imecheza mechi 26 na imevuna pointi 50 ikiwa nafasi ya tatu.
Shughuli itakuwa nzito kwenye vita ya utupiaji ambapo Namungo itamkosa mshambuliaji wake namba moja Relliants Lusajo mwenye mabao 11 lakini balaa lipo kwa Bigirimana Blaise ambaye ametupia mabao 9 akimpoteza David Molinga wa Yanga mwenye mabao nane.
Namungo ni hatari kwa kushambulia ambapo kwenye mechi zao 27 sawa na dk 2,430 walizocheza wamefunga mabao 33 wakiipoteza Yanga ambayo kwenye mechi 26 sawa na dk 2,340 walizocheza wamefunga mabao 30.
Ubovu wa Namungo ni kwenye beki ambapo wamekubali kufungwa mabao 24 huku Yanga ikifungwa mabao 19 jambo litakalomaliza ubishi leo ni dk 90.
Hitimana Thiery, Kocha wa Namungo alisema kuwa wapo tayari kwa ushindani na wanahitaji pointi tatu huku Luc Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga akisema kuwa watapambana kupata matokeo.
0 Comments