SVEN AWATAKA YANGA MICHUANO YA FAUkweli ni kwamba mpaka leo Mkufunzi wa Simba Sven Vandenbroeck bado haamini kama timu yake ilishindwa kuibuka na ushindi kwenye mechi zote mbili za Ligi dhidi ya Yanga msimu huu

Sven aliyeanza majukumu ya kuinoa Simba mwezi Disemba 2019, aliwaongoza mabingwa hao wa nchi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga uliopigwa Januari 04 2020 akishuhudia timu yake ikipoteza uongozi wa mabao mawili na kulazimishwa sare ya 2-2

Lakini pia Machi 08 akaishuhudia timu yake ikipoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0 katika mchezo ambao Simba ilitengeneza nafasi nyingi na kutawala mchezo kwa muda mwingi
Pamoja na timu yake kujihakikishia ubingwa wa tatu mfululizo, Sven amesema anatamani apate nafasi nyingine ya kucheza na Yanga kwenye michuano ya kombe la FA

"Ukifuatilia mechi zote mbili tulizocheza nao, tulikuwa bora zaidi nayo na inakuwa ngumu sana kuamini kuwa tulishindwa kupata matokeo. Nadhani jambo pekee ambalo walikuwa nalo kwenye mechi zile ni bahati,"

alisema Sven ambaye yuko mapumziko baada ya ligi kusimama kutokana na janga la virusi vya Corona

"Wakati mwingine matokeo yasiyotarajiwa hutokea.. Kikosi changu kiko tayari kucheza nao kwa mara nyingine hasa ikitokea tumekutana kwenye michuano ya kombe la FA"

Simba na Yanga zote zimetinga robo fainali wakisubiri droo ya hatua hiyo ambayo itafanyika baada ya April 17

Post a Comment

0 Comments