Inaelezwa hesabu za Yanga ni kuongeza washambuliaji wawili matata ambao wataiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji.Mchakato wa kumrejesha Herietier Makambo anayeitumikia Horoya Ac ya Guinea tayari umeshaanza lakini pia mabingwa hao wa kihistoria wametupia jicho pale Azam Fc kwani pana mchezaji wao, Obrey Chirwa
Ndio! baada ya kuondoka Yanga, Chirwa alikwenda Misri ambako alijiunga na timu ya daraja la kwanza lakini akaikacha baada ya miezi mitatu tu
Akaomba sana afikiriwe kurudi Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita
Pamoja na uongozi wa Yanga kuridhia mshambuliaji huyo raia wa Zambia asajiliwe, akakutana na kikwazo cha kocha Mwinyi Zahera ambaye aligoma kumpa mkataba kwa kuhofia ile tabia yake ya migomo pale anapocheleweshewa haki zake
Hata usajili uliopita Chirwa alisaini mkataba mpya Azam Fc dakika za mwisho baada ya jitihada za kurejea Jangwani kukwama tena
Chirwa aliyeifungia Azam Fc mabao nane msimu huu, mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu
Inaelezwa kocha Luc Eymael amevutiwa na aina yake ya uchezaji na anadhani anaweza kukinufaisha kikosi chake ambacho kitakuwa kimejaa mafundi kwelikweli
Kama mipango yote ya usajili ya Yanga itakamika, basi safu yake ya ushambuliaji itakuwa na Bernard Morrison, Ditram Nchimbi, Obrey Chirwa, Heritier Makambo na Tariq Seif
Hapa ukame wa mabao utabaki kuwa historia...!
0 Comments