Baada ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga Heritier Makambo kutamka bayana kuwa anatamani kurejea Tanzania kuwatumikia tena mabingwa hao wa kihistoria, mashabiki wa Yanga wameipokea kwa furaha kauli hiyo ya Mcongomani huyo ambaye kwa sasa anaitumikia Horoya Ac ya Guinea
Yanga ilimuuza Makambo msimu uliopita kwenda Horoya AC kwa kitita cha zaidi ya Tsh Milioni 180, kocha wa zamani wa timu hiyo Mwinyi Zahera akihusika kwa kiasi kikubwa kwenye mauzo hayo
Wakati anaondoka Yanga, Makambo alikuwa bado na mkataba wa mwaka mmoja
Hata hivyo mshambuliaji huyo aliyeifungia Yanga mabao 23 kwenye mashindano yote katika msimu wake wa kwanza, ni kama aliondoka na mabao yote kwani msimu huu Yanga imekuwa na changamoto kubwa kwenye safu ya ushambuliaji
Yanga inaweza kuweka rekodi ya msimu ambao imefunga mabao machache katika kipindi cha miaka 10 iliyopita
Na sasa wadau wametaka kuona uongozi unachukua hatua mapema kwa kusajili washambuliaji ambao hawatakuja kwa majaribio kama ilivyokuwa kwa nyota wengi waliosajiliwa msimu huu
Ujio wa Sadney Urikhob, Juma Balinya na David Molinga haujakuwa na msaada kwa Yanga
Kwani hata ukijumlisha mabao yao yote waliyoifungia Yanga hawafikii hata nusu ya mabao aliyofunga Makambo
Makambo ni mshambuliaji ambaye ameacha alama Yanga, hivyo kama uongozi utafanikiwa kumrejesha, utakuwa ni uamuzi sahihi sana
Mashabiki wanamfahamu, wanampenda na hata yeye mwenyewe ametamka wazi kuwa Yanga ni kama nyumbani kwake na anaamini atarejea siku moja
Pamoja na kuwa bado ana mkataba wa miaka miwili na Horoya, Makambo amesema kama mazungumzo yatafanyika kati ya Yanga na timu yake kisha makubaliano yakafikiwa, yuko tayari kurejea Jangwani hata kesho
0 Comments