Baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema matokeo hayo mazuri waliyopata yalitokana na kufanyia kazi mapungufu ya kikosi cha Simba
Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Bernard Morrison, ambaye alimtungua kipa wa Simba, Aishi Manula kwa mpira wa adhabu uliozama wavuni baada ya kuchezewa rafu na Jonas Mkude nje kidogo ya eneo la 18.
Eymael amesema alikuwa akiwafuatilia wapinzani hao mara kadhaa walipokuwa wakicheza na kufanyia kazi ubora na mapungufu ya kikosi chao.Eymael amebainisha kuwa kitu alichofanikiwa ni kuidhibiti safu ya kiungo ambayo mechi zake tatu zilizopita, Simba ilicheza vizuri ikiongozwa na Mzambia Clatous Chama na Mkenya Francis Kahata.
"Vijana wangu wamecheza vizuri, wamefanyia kazi yale yale tuliyokuwa tukifanya mazoezini na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wetu huu dhidi ya Simba, ila haikuwa mechi rahisi," alisema Eymael.
Mbelgiji huyo alisema baada ya matokeo hayo, wanaenda kujipanga kwa mara nyingine kwenda kutafuta pointi tatu muhimu katika mchezo wa ligi hiyo unaofuata dhidi yaKMC.
"Nina furaha na kumshukuru Mungu kwa kupata ushindi dhidi ya Simba, hatukucheza kama 'dabi', tulicheza kama fainali, ingawa tulipoteza nafasi kadhaa, kama ile ya Nchimbi (Ditram) na Kaseke, lakini tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye michezo iliyobaki.
0 Comments