Klabu ya KMC imemtangaza rasmi Kali Ongala kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Moarin aliyevunja mkataba na klabu hiyo. Hii ni mara ya kwanza kwa Ongala kuwa kocha wa kudumu
Je Kali Ongala ni nani?
Kali Ongala alizaliwa 31 Agosti 1979 jijini London nchiniUingereza na baba yake mzazi ni aliyewahi kuwa Mwanamuziki mashuhuri nchini Tanzania Remmy Ongala. Mwaka 1999 alianza safari ya kusakata kabumbu katika klabu ya Yanga . Mwaka 2005-2007 aliitumikia Vasby United ,Msimu wa 2007-2010 alijiunga na GIF Sundsvall na 2010 aliitumikia Umea FC na baadaye kutimkia Azam Fc alikodumu kwa msimu mmoja mpaka 2011. Kustaafu kwa Kai Ongala kulipelekea nyota huyo kupewa majukumu ya kocha msaidizi akishirikiana na Steward Hall.
Je Ongala ni chaguo sahihi kwa KMC?
2 Julai 2022 Klabu ya Azam ilimtambulisha rasmi Kali Ongala kuwa kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili(Fitness Coach) na baadaye alikaimu nafasi ya kocha mkuu wa mpito akiiongoza Azam katika michezo 32 alishinda michezo 21 sare 4 na kupoteza michezo 7.
Msimu wa 2022/23 Kali Ongala aliiongoza Azam FC kuingia fainali za kombe la Azam Sports Federation akicheza michezo 6 na kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Yanga. Tarehe 14 Julai 2023 klabu ya Azam ilitangaza kuachana na Kali Ongala na nafasi yake kuchukuliwa na Youssuf Dabo .
Mara baada ya kuachana na Azam FC kocha huyo aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana U20 na mpaka anateuliwa na KMC alikuwa katika majukumu ya timu hiyo
Rekodi nzuri alizoweka Kali Ongala ndani ya Azam FC zinatuaminisha atafanya mambo makubwa ndani ya KMC ikizingatiwa kwamba timu ina wachezaji wenye uwezo mkubwa ingawa haijafanya vizuri kwenye ligi baada ya kushinda michezo 4 kupoteza michezo 5 na sare 2 hivyo kuangukia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 14.
Kauli ya Ongala baada ya kutambulishwa KMC
”Napenda kuushukuru uongozi wa KMC kwa kunipa nafasi katika klabu hii ,Kwangu ni fursa ya kipekee sana na naamini hapa ni sehemu sahihi kuendelea kukuza taaluma yangu ya ukocha nikishirikiana na benchi la ufundi.Nilikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana (U20) kwa namna KMC walivyonipa mpango kazi wao nimeshawishika kujiunga nao mbali na kwamba nilipokea ofa nyingi”
0 Comments