Klabu ya Simba imerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu NBC baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya KMC. Aliyekuwa mchezaji wa zamani wa KMC ,Awesu awesu ndiye aliyefungua lango la KMC kwa bao safi akimalizia pasi kutoka kwa Steven Mukwala dakika ya 25.
Dakika ya 38 Simba walipata penati iliyopigwa na Jean Charles Ahoua na mpira kwenda mapumziko Simba wakiongoza kwa mabao 2-0. Mabadiliko ya kuingia kwa Edwin Balua yalizaa matunda kwa Simba baada ya kupachika bao la 3 dakika ya 66 ya mchezo na Ahoua alirejea tena langoni kwa kufunga bao la nne dakika ya 69.
Matokeo hayo yanawafanya Simba kufikisha alama 25 katika michezo 10 waliyocheza mpaka sasa.Ubora wa safu ya ushambuliaji umeifanya Simba kufunga mabao 21 na kufungwa mabao matatu pekee katika mechi hizo.
Jean Charles Ahoua ameendelea kuwa gumzo ndani ya Simba baada ya kuhusika katika magoli 9 akifunga mabao 5 na kutengeneza mengine 4. Mashabiki wengi wa Simba wanaamini nyota huyo atafanya mambo makubwa ndani ya ligi yetu na kuna uwezekano mkubwa akawa mchezaji bora wa msimu huu akirudia alichokifanya ligi ya Ivory Coast msimu wa 2023/24
0 Comments