Nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto na rafiki yake, Zawadi Mauya wa Singida Black Stars wamemshika mkono aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu kwa kumchangia Sh1 milioni kupitia mfuko wao wa hisani wa Mwamnyeto Foundation.
Akizungumza kwa niaba ya nyota hao, Carlos Sylivester ‘Master Mind’ ambaye pia ni meneja wa wachezaji hao wakati akikabidhi kiasi hicho, alieleza namna ilivyokuwa hadi kupata taarifa za kile kinachoendelea kwa mchezaji huyo.
“Nilikuwa nje ya nchi nilivyoona ile video kupitia mitandao ya kijamii, usiku ule ule niliwasiliana na Zawadi Mauya ambaye aliniambia kaka lazima tufanye kitu na kwa bahati nzuri mwenzangu alikuwa na ukaribu na aliyeripoti habari hiyo.
“Sisi kama taasisi tuliamua kufanya kitu kwa sababu taasisi ipo kwa ajili ya kurudisha kwa jamii,” anasema Master Mind ambaye alifuatana na mwekahazina, John Majollo na meneja wa taasisi hiyo, Herman Massepo.
Wakiwa nyumbani kwa Mdamu, Master Mind aliendelea kuongea kwa kusema; “Tupo hapa kuhamasisha na kufungua milango kwa wengine nao waweze kusaidia, sisi tumeitikia wito wa Mwananchi na tunaita wadau wengine.
“Tunajua kuwa matibabu yatafanyika, lakini kwa muda mrefu utakuwa ukitibiwa kwa hiyo nje na matibabu nini kinafuata kwa hiyo sisi kama taasisi tukaona tukuchangie kidogo (alimweleza Mdamu).”
Kwa upande wake, Mdamu aliwashukuru Mwamnyeto na Mauya kwa mchango wao kwake; “Nimekuwa nikiumia sana na kitendo kuwa naombaomba, nahitaji kusimama mwenyewe na kuchakarika.”
Julai 9, mwaka 2021 basi lililobeba wachezaji timu ya soka ya Polisi Tanzania, lilipata ajali wakati wakitoka mazoezini kwenye Uwanja wa TPC kwenda kambini, Mdamu alivunjika miguu yote miwili, akapelekwa katika hospitali ya KCMC, Moshi kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Miaka mitatu tangu ajali ile, mchezaji huyo ambaye mkataba wake na Polisi Tanzania ulimalizika akiwa anaendelea kujiuguza majeraha ya ajali hiyo, bado hajapona baadhi ya vidonda vya upasuaji aliofanyiwa vingine vikitoka usaha, huku daktari aliomfanyia upasuaji wa kwanza akimpa taarifa nyingine mbaya kwamba hataweza kucheza soka tena maishani.
Nyota huyo anahitaji anahitaji sapoti ili kufanyiwa upasuaji mwingine huku hali yake ya kiuchumi ikianguka jambo linalofanya yeye na familia yake ya watoto wawili na mkewe kulazimika kula mlo mmoja kwa siku wakati mwingine.
0 Comments