Simba wamegonga hodi tena kwa Winga Mkongoman Elie Mpanzu, winga huyo aliyekuwa akiichezea AS Vita kabla ya kutimkia Ubelgiji, aliwahi kuhitajika na Simba lakini aliamua kuwakacha kweupe akitoa sababu za kufanya hivyo ikiwamo ishu ya familia, lakini mabosi wa Msimbazi wameamua kumrudia tena huko huko Ulaya.
Inaelezwa Simba imerejea tena kwa winga huyo, baada ya kuona kikosi hicho kinahitaji nguvu hasa eneo la kushoto, na mchezaji huyo kuonekana kama amechemka huko Ubelgiji.
Taarifa za ndani kutoka klabu ya Simba zinaeleza kuwa, hatua ya kumrudia Mpanzu imetokana baada ya kugundua kuwa kuna mahali panavuja hasa eneo la winga.
“Kuna mchezaji mmoja itabidi atolewe kama dili la Mpanzu litatiki ili kutimiza kanuni ya kuwa na wachezaji 12 wa kigeni. Hatuwezi tukasema atakuwa nani kwani bado ni mapema lakini kocha ndiye mwenye maamuzi juu ya hili, hivyo ataongea na uongozi juu ya nani apunguzwe,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.
Hatua ya Simba kumrudia Mpanzu wanaona bado kikosi chao hakina nguvu kwa winga ya kushoto wakati mwenye asili ya kulia akiwa Joshua Mutale, huku kukiwa na wachezaji wengine kama Kibu Denis, Ladack Chasambi na Edwin Balua ambaye kuna wakati anachezeshwa upande huo wa kushoto.
Mpanzu anaweza kucheza eneo la ushambuliaji na kama atanaswa basi uwezekano wa Steven Mukwala kuendelea kuwa mshambuliaji kiongozi basi itakuwa ngumu kwake.
0 Comments