BETI NASI UTAJIRIKE

Nani yuko nyuma ya sajili tata za Simba

 Nani yuko nyuma ya kamati ya usajili Simba? Hili ni swali ambalo kila mwanasimba anapaswa kujiuliza wakati huu ambao dirisha la usajili limebakiza siku moja tu kuweza kufungwa. Mwekezaji na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Bw.Mohammed Dewji ndiye anayeweza kutusaidi kutupa majibu haya. 


Sote tumeshuhudia namna Simba ilivyofanya usajili wa wachezaji wengi wa kigeni na wazawa,sote tuliamini sajili hizo zimefuata taratibu zote za kisheria kuanzia kwa mchezaji binafsi na klabu anayotoka lakini mambo yamekuwa tofauti kwa baadhi ya sajili baina ya wachezaji na timu walizotoka.

Usajili wa Lameck Lawi 

Beki wa kati kutoka Coastal Union alikuwa ndiye nyota wa kwanza kabisa kutangazwa na Simba mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa. Simba walimtangaza mchezaji huyo kupitia mitandao ya kijamii lakini Coastal Union walijitokeza hadharani na kukana kwamba klabu haijahusishwa  na usajili huo na  kwamba nyota huyo hajauzwa na ni mali halali ya Coastal Union kwa sababu bado ana mkataba na klabu hiyo.

Baada ya Coastal kutoa waraka wake hatukuona majibu yoyote kutoka kwa Simba.Baadaye nyota huyo alisafiri kwenda Ubelgiji kwa ajili ya majaribio na mpaka sasa hatma yake haijawekwa hadharani kama alifaulu majaribio au alishindwa lakini pia hajaonekana kambini kwa Coastal Union wala Simba.

Usajili wa Awesu Awesu

Kiungo huyu mshambuliaji alitangazwa na klabu ya Simba na alisafiri na timu kuelekea Misri walikoweka kambi .Mara baada ya kurejea alicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya APR siku ya Simba Day na wengi tukaaminishwa amekwishasajiliwa na wekundu wa msimbazi. KMC FC walitoka hadharani na kudai Awesu Awesu ni mali yao halali  anamkataba na klabu hiyo yenye makao yake makuu Mwenge Kinondoni Dar es salaam. Shauri lilipelekwa TFF na klabu hiyo ilipata ushindi baada ya kutoa ushahidi wa malalamiko yao. Mpaka sasa Awesu Awesu ni mali ya KMC na imebaki siku moja dirisha kufungwa na kama Simba wanamhitaji kiungo huyo basi wanapaswa kufuata taratibu zote za kiusajili kwa kumalizana na wana kinondoni.

Sekeseke la Israel Mwenda 

Kijana chipukizi aliyefanya vizuri msimu uliopita ndani ya Simba SC.Tarehe 25 June 2024 aliongezewa mkataba wa miaka miwili ndani ya klabu hiyo . Mkataba huo ungemweka mchezaji huyo mpaka tarehe 30 juni 2026. Hapo jana Klabu ya Simba ilitoa taarifa rasmi kwa mashabiki wake kwamba wamemruhusu nyota huyo akatafute changamoto mpya sehemu nyingine  kwa maslahi ya kipaji chake. Mara baada ya taarifa hiyo kutoka mchezaji huyo alitumia mitandao yake ya kijamii kuonyesha kwamba amesajiliwa na klabu nyingine. Swali la kujiuliza ni ilikuwaje Simba wakamwongeza mkataba nyota huyo na baada ya muda wakaachana naye? Je mchezaji huyo ameuzwa au amevunja mkataba wake yeye mwenyewe?

Maswali kwa ishu ya Kibu Denis

Kibu Denis aliibua sintofahamu mara tu alipokamilisha kusaini kandarasi mpya ya kuitimikia Simba. Nyota huyo hakuonekana kambini Misri na baadaye taarifa zilisema ameenda kufanya majaribio Ubelgiji bila kuwa na ruhusa ya klabu. Siku ya Simba Day nyota huyo alicheza mchezo dhidi ya APR na msemaji wa Simba Ahmed Ally aliwasihi wanasimba kumsamehe mchezaji huyo na klabu ingemchukulia hatua za kinidhamu. Sote tunatakiwa kuhoji je ni nani alikuwa nyuma ya sakata la kibu denis? na kama angefanikiwa kupata timu Ubelgiji klabu ingenufaika na ada ya usajili?

Yuko wapi Aishi Manula

Yuko wapi Tanzania One Aishi Manula? Nyota huyo hajaonekana ndani ya Simba tangu Novemba 5 siku ambayo Simba ilifungwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga na Manula ndiye alikuwa goli kipa. Tangu wakati huo mchezaji hajaonekana kambini na hata wakati wa maandalizi ya msimu mpya pale Misri hakusafiri na timu. Siku ya Simba Day klabu hiyo iliwatangaza magolikipa wake wanne watakaotumika msimu wa 2024/25 na kati ya hao jina la Manula halikuwemo.  Taarifa za awali zinasema kuwa nyota huyo bado anamkataba na Simba na amehusishwa kutua Azam FC ikiwa imesalia siku moja . Swali pekee tunalopaswa kuhoji ni Simba wanampango gani na Manula kwa msimu huu? kama hawamuhitaji kwanini wasimuuze ama kumtoa kwa mkopo? kwanini sakata lake linazua sintofahamu wakati ni mchezaji wa viwango vya juu na ni mzoefu .

Kamati ya usajili ya Simba inatupa maswali mengi mno kujua ni wapi wanaelekea msimu huu. Nimetafakali usajili wa kipa Camara kisha nimetafakali ujio wa mshambuliaji mpya Lionel. Kwanini klabu kubwa kama hii inafanya mambo yake kwa kuzima moto? kwanini wasingefanya tathmini wakati ule timu inafanya vibaya na nyakati hizi za usajili wangefanya mambo kwa wepesi tu.

 


Post a Comment

0 Comments