Simba SC wameibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kirafiki kuhitimisha tamasha la Simba Day na Wiki ya Mabingwa hao kwa ujumla jon ya leo Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Imekuwa kawaida kwa mwaka wa 12 sasa, Simba SC kuzindua msimu mpya kwa tamasha kubwa linalopambwa na burudani ya muziki kabla ya kutambulisha kikosi cha msimu kwa mchezo wa kirafiki. Na leo baada ya burudani zilizoongozwa na msanii nyota zaidi nchini, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ukawadia mchezo huo wa kirafiki, ambao kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kiliwapa furaha mashabiki wao. Hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa 2-0, kazi nzuri ikifanywa na kiungo mpya wa kimataifa wa Zambia, Rally Bwalya akiseti mabao yote hayo.Morrison alifunga bao la kwanza dakika ya 44 kwa shuti la mguu wa kulia kufuatia pasi ndefu na nzuri ya mchezaji wa zamani wa Power Dynamos ya Zambia, Bwalya. Morrison naye akapokea pasi nyingine nzuri ya Bwalya na kumtilia krosi nzuri ya chini Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco aliyefunga bao la pili dakika ya za nyongeza kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili kocha wa Simba SC, Mbelgiji Sven-Ludwig Vandenbroeck alibadili kikosi kizima ambacho kilikwenda kutanua ushindi hadi mabao sita. Kiungo mwingine Mzambia, Clatous Chotta Chama alifungua shangwe za mabao kipindi cha pili kwa kufunga la tatu dakika ya 56 baada ya kumlamba chenga beki wa Vital’O na kufumua shuti kufuata krosi nzuri ya Ibrahim Ajibu Migomba kutoka kulia. Ajibu mwenyewe akafunga bao la nne dakika ya 76 akimalizia pasi ya Chama, kabla ya mchezaji mwingine mpya, mshambuliaji Mkongo Chriss Mugalu aliyesajiliwa kutoka Lusaka Dynamos kufunga la tano dakika ya winga mpya Charles Ilamfya aliyesajiliwa kutoka KMC ya Kinondoni akaitelezea krosi ya chini ya Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kutoka upande wa kushoto kufunga bao la sita dakika ya 90 . Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula/Beno Kakolanya dk46/Ally Salim dk69, Shomari Kapombe/David Kameta dk46, Gardiel Mchael/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk46, Ibrahim Ame/Kennedy Willson dk46, Joash Onyango/Gerson Fraga dk46, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk46, Hassan Dilunga/Ibrahm Ajibu dk46, Rally Bwalya/Clatous Chama dk46, John Bocco/Chris Mugalu dk46, Said Ndemla/Miraj Athuman ‘Madenge’ dk46 na Bernard Morrison/Charles Ilamfya dk46.
0 Comments