BETI NASI UTAJIRIKE

UCHAMBUZI: MAMBO UNAYOPASWA KUYAJUA LEO MCHEZO WA AZAM VS YANGA

Ni Azam vs Yanga hii leo dimba la taifa jijini Dar es salaam . Timu hizi hazigombei nafasi ya pili tu lakini heshima ndani ya Dar es salaam. Azam na Yanga wamekuwa na historia nzuri kila wanapokutana na mara zote matokeo ya mechi hizo huwa ni ngumu kutabirika kutokana na umahiri wao.Timu zote zinanolewa na makocha kutoka bara la Ulaya .Azam FC inaongozwa  na Aristica Cioaba raia wa Romania na Yanga ipo chini ya Kocha Mkuu Luc Eymael raia wa Ubelgiji.
Rekodi za Azam vs Yanga 

Vita yao kubwa itaamuliwa baada ya dakika 90 huku  hawa jamaa ambao balaa lao uwanjani lipo namna hii watafanya yao:-
Wakali wa asisti
Azam FC yupo beki wa kulia, Nicolas Wadada ambaye ana jumla ya pasi saba za mabao kati ya mabao 39 yaliyofungwa kwenye mechi 29 za ligi ambazo ni dakika 2,610.
 Amecheza mechi 23, ambazo ni sawa na dakika 2,070 pia ana bao moja kibindoni.Yanga tegemeo lao ni Juma Abdul ambaye ni nahodha msaidizi. Yanga ikiwa imecheza jumla ya mechi 29 na kufunga mabao 33 amehusika kutengeneza jumla ya pasi tano za mabao.Pasi zake zote tano Abdul amezimwaga kwa kutoka pembeni akitumia guu lake la kulia.
Wakali wa kucheka na nyavu
Obrey Chirwa ni kinara wa kutupia ndani ya Azam FC, ametupia jumla ya mabao nane. Mbali na kutupia pia ni mzuri kutengeneza nafasi za mabao ambapo ametengenza jumla ya pasi tatu na kumfanya ahusike kwenye mabao 11 kati ya 33 yaliyofungwa na Azam msimu huu.
David Molinga ni kinara kwa utupiaji ndani ya Yanga ambapo ametupia jumla ya mabao nane kati 33.
Wachezaji wa kuchungwa
Idd Seleman,’Naldo’ nyota huyu mzawa ndani ya Azam FC moja ya sifa iliyowavutia Azam FC kumng’oa ndani ya Mbeya City ni pamoja na kuwa na uzoefu wa mechi ngumu hasa za Simba na Yanga.Akiwa na mabao matano kibindoni baada ya kucheza mechi 20 akiwa ndani ya uwanja sio wa kuachwa Aishi Manula wa Simba anaijua shughuli yake.
Sure Boy
Salum Abubakar, ‘Sure Boy’  ni mpole akiwa ndani ya uwanja ila mjanja kulitazama lango na kutengeneza hatari.Kiungo huyu amecheza jumla ya mechi 24 na ametengeneza pasi tatu za mabao.
 Balama
Mapinduzi Balama wa Yanga yeye ni mwana mapinduzi akiwa ndani ya uwanja hasa kwenye mechi ngumu. Kibindoni ana mabao matatu na ana uwezo wa kufunga mabao ya umbali wa mita 20.
Nchimbi
Ditram Nchimbi ni mshambuliaji mwenye kutumia nguvu nyingi, anaitambua falsafa ya Azam FC kwa kuwa alikuwa mchezaji wao zamani. Kibindoni ana jumla ya mabao sita akiwa amefunga mawili ndani ya Yanga na manne alifunga alipokuwa Polisi Tanzania.
Niyonzima
Haruna Niyonzima, ni mchezaji ambaye amekuwa ni mhimili wa timu kwa kuituliza na kuanzisha mashabulizi.Uzoefu wake kwenye mechi ngumu na kubwa unambeba.
Watakaokosekana
Razack Abarola, mlinda mlango namba moja wa Azam FC. Daniel Amoah na Yakub Mohamed wataukosa mchezo wa leo kwa kuwa wapo nchini Ghana ambapo mipaka bado imefungwa kutokana na kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.
Lamine Moro beki kisiki wa Yanga ana adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata Juni 17 Uwanja wa Jamhuri kwa kitendo chake kisicho cha kiuungwana kwa kumchezea rafu, Mwinyi Kazimoto wa JKT Tanzania. Papy Tshishimbi nahodha wao na  Ally Mtoni ‘Sonso’ beki bado hawajawa fiti. Ally Ally na Erick Kabamba hawapo kwenye mpango wa Kocha Mkuu Luc Eymael kwa sasa.
Mechi zao za hivi karibuni
Azam FC ilishinda mabao 2-0 mbele ya Mbao FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Chamazi huku Yanga ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na JKT Tanzania Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Walipokutana kabla ya janga la Virusi vya Corona, Januari 19, Azam FC ilishinda bao 1-0 Uwanja wa Taifa, bao ambalo alijifunga beki Ally Mtoni,’Sonso’.
Wakali wa mipira iliyokufa
Azam FC ina wakali watatu wa kutumia mipira iliyokufa.Richard Djod ambaye kibindoni ana mabao manne alifunga bao moja kwa penalti.Agrey Morris ambaye ni nahodha ana bao moja ambalo alifunga kwa penalti pamoja na Nevere Tigere mwenye mabao matatu moja alifunga kwa faulo.
Yanga wao mkali wao ni David Molinga ambaye amefunga mabao matatu kwa mipira iliyokufa. Amefunga kwa faulo mabao mawili na amefunga kwa penalti bao moja.Patrick Sibomana ametupia mabao sita na ana bao moja alilofunga kwa mpira wa faulo ilikuwa mbele ya Ndanda FC kwa guu lake la kushoto.
Vita ya nafasi
Timu zote mbili kwa sasa zinagombania nafasi ya pili ambapo ikiwa Azam FC itashinda itajihakikishia ufalme kwenye nafasi hiyo kwani wameachana kwa pointi mbili pekee wakiwa na pointi 57. Yanga ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 55 huku zote zikiwa zimecheza mechi 29.

Post a Comment

0 Comments