BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI:HIVI NDIVYO JKT TANZANIA ILIVYOWABANA YANGA

Klabu ya Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana 1-1 na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.


Matokeo hayo yanaiongezea pointi moja kila timu, Yanga ikifikisha 55 katika mchezo wa 29 na kubaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 57 na Simba SC pointi 72 za mechi 29 – wakati JKT Tanzania inafikisha pointi 43 katika mchezo wa 29 pia na inabaki nafasi ya saba.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ludovic Charles wa Mwanza aliyesaidiwa na Abdulaziz Ally wa Arusha na Japhet Kasiliwa wa Sumbawanga, hadi mapumziko JKT Tanzania walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na beki wa pembeni wa timu hiyo, Michael Aidan Pius dakika ya 36 kwa shuti la umbali wa mita 35 na ushei akiupitisha mpira juu ya kipa Metacha Boniphace Mnata kufuatia pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula.

Iliwachukua dakika 40 za kucheza Yanga SC kuweza kusawazisha bao hilo, mfungaji akiwa ni Patrick Sibomana dakika ya 76 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mohammed Abdulrahman ‘Wawesha’ kufuatia shuti la kiungo mwenzake wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima.

Mechi ‘ikachafuka’ baada ya bao hilo, JKT Tanzania wakicheza kwa kutumia nguvu zaidi kujizuia kuruhusu bao lingine huku Yanga SC wakitafuta bao la ushindi.

Refa Ludovic Charles alilazimika kuwatoa kwa kadi nyekundu, beki Mghana wa Yanga SC Lamine Moro na kiungo mzawa wa JKT, Mwinyi Kazimoto dakika ya 89 baada ya wawili hao kupigana kufuatia kutokea tafrani baina ya wachezaji wa timu zote mbili uwanjani.

Tafrani hiyo ilianza baada ya mabeki wa JKT Tanzania kumuangusha na kumtimba Sibomana, hivyo wachezaji wa Yanga kuingilia kati na ndipo Moro alipokwenda kumpiga teke Kazimoto ambaye alimkimbiza Mghana huyo kutaka kumrudishia, lakini akawahiwa na kuzuiwa.    

Awali, dakika ya 49 msaidizi namba mbili wa refa, Japhet Kasiliwa wa Sumbawanga alikataa bao la Yanga lililofungwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ akimalizia mpira uliotemwa na kipa Wawesha kufuatia mshambulaji Ditram Nchimbi kuunganisha krosi ya kiungo Deus Kaseke kutoka upande wa kushoto. 

Kikosi cha JKT Tanzana kilikuwa; Mohammed Abdulrahman ‘Wawesha’, Michael Aidan, Abdallah Waziri, Frank Nchimbi, Edson Katamba, Jabir Aziz, Mwinyi Kazimoto, Kelvin Nashon/Mohammed Rashid dk63, Shaaban Mgandila/ Hafidh Mussa dk70, Hassan Materema na Adam Adam.

Yanga SC; Metacha Mnata, Juma Abdul, Adeyoum Ahmed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Haruna Niyonzima/ David Molinga dk81, Mapinduzi Balama/Patrick Sibomana dk52, Ditram Nchimbi na Deus Kaseke/ Yikpe Gislain dk68.

Post a Comment

0 Comments