ads

adds

HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOICHAKAZA MWADUI MABAO 3-0 UWANJA WA TAIFA


Klabu ya Simba imezidi kujisogeza karibu na taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Mwadui FC kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck inafikisha pointi 75 baada ya kucheza mechi 30, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 15 zaidi ya Azam Fc inayofuatia nafasi ya pili. 

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hance Mabena aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na  Hamdani Said wote wa Tanga, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa na kiungo Hassan Dilunga dakika ya tisa akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji na Nahodha, John Raphael Bocco na beki Augustino Simon aliyejifunga dakika ya 21 akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na beki Shomari Kapombe kutoka upande wa kulia.
Kipindi cha pili Mwadui FC walirudi na maarifa mapya na kufanikiwa kuwazuia Simba SC kupata mabao zaidi, lakini haikuwasaidia.

Nahodha John Bocco akawainua wapenzi wa Simba SC dakika ya 58 akifunga bao la tatu akimalizia kwa kichwa mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la nyota kutoka Msumbiji, Luis Miquissone aliyepokea pasi ya Said Ndemla.  

Post a Comment

0 Comments