Beki na nahodha wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto amefungukia usajili wake wa kutua Simba ambapo kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na timu hiyo.Tangu usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu, beki huyo ilielezwa kuwa, amesaini mkataba wa awali wa kuitumikia Simba, akisubiri msimu uishe ajiunge na timu hiyo.
Baada ya tetesi kuwa nyingi, hivi karibuni taarifa mpya zilitoka kwamba, tayari Simba imetoa gari na kiasi cha Sh milioni 85 kumchukua beki huyo, huku mwenyewe akiwa bado hajazungumza chochote juu ya usajili wake huo.
Alipotafutwa beki huyo mahiri na tegemeo wa Coastal alikiri kuwa Simba wamemfuata wakitaka kumsajili lakini bado kuna vitu havijakamilika, hivyo wakifikia muafaka basi anamwaga wino Msimbazi.
"Ni kweli Simba wamenifuata na kuhitaji huduma yangu, mimi nipo tayari kwenda Simba kama tutafikia muafaka mzuri na kutimiza mahitaji yangu kwa sababu mpira mimi ndiyo kazi yangu kwa hiyo naweza nikacheza popote pale, siyo Simba pekee," alisema Mwamnyeto.
0 Comments