Kumekuwa na mjadala mkali miongoni mwa wadau wa klabu ya Yanga wengi wakionekana kutofurahishwa na kitendo cha nahodha wao Papy Tshishimbi 'kusuasua' kusaini mkataba mpya
Hivi karibuni Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli alidokeza kuwa Tshishimbi alipewa ofa nono hivyo wanaamini atasaini mkataba huo hasa ikizingatiwa kocha Luc Eymael amependekeza Mcongoman huyo abaki
Lakini hata ikitokea Tshishimbi akaondoka Yanga, mabingwa hao wa kihistoria sidhani kama watatetereka
Miongoni mwa wachezaji wanaohusishwa kuchukua nafasi yake ni kiungo mkabaji wa Mtibwa Sugar Abdulkarim Humud
Kama Yanga itafanikiwa kumpata mwamba huyu, basi Wanayanga watamsahau Tshishimbi haraka sana Iko hivi, kwa mfumo ambao kocha Luc Eymael anatumia sasa, majukumu ya Tshishimbi yako zaidi kwenye kuilinda safu ya ulinzi, na wakati mwingine kuanzisha mashambulizi
Ukiangalia kwenye mchezo dhidi ya Simba ambao Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Eymael alibadili mfumo wake kutokana na aina ya wachezaji aliokuwa nao na hii inatoa taswira ya mwelekeo wa Yanga jinsi itakavyokuwa ikicheza
Ukiangalia katika mechi ile aliyen'gara zaidi kwenye safu ya kiungo ni Feisal Salum 'Fei Toto'. Fundi huyu wa mpira kutoka visiwani Zanzibar pengine ndiye aliyepata alama nyingi zaidi miongoni mwa viungo wote wa Yanga na Simba waliiocheza siku ile
Fei Toto alikuwa hatari kwelikweli, ndio maana kuna wakati Clatous Chama alimfanyia madhambi ya makusudi kabisa, tukio ambao pengine lingeweza kumaliza maisha yake ya kusakata kabumbu
Huyu Fei Toto kwa sasa mfukoni mwake ndio anatembea na ramani yote ya mchezo wote wa Yanga
Baada ya Eymael kubaini ni mchezaji fundi kwelikweli, mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi makini tena hata akiwa umbali mrefu, amempa jukumu hilo zito
Eymael anamtumia Fei Toto kama kiungo mkabaji 'fake' lakini kazi yake kubwa ni kuchezesha timu kutokea nyuma akishirikiana vyema na Haruna Niyonzima anayecheza juu yake
Kwenye mchezo dhidi ya Simba alicheza chini pamoja na Tshishimbi lakini yeye jukumu lake kubwa lilikuwa kuanzisha mashambulizi pale wanapopora mpira.Kazi zote 'chafu' zilikuwa zikifanywa na Tshishimbi, Toto yeye alitumika zaidi Yanga inapokuwa na mpira, uwezo wake wa kupiga 'pasi rura' ilikuwa silaha muhimu
Turudi kwa Humudi
Humud amekuwa na msimu bora sana klabu ya Mtibwa Sugar, haishangazi kuona kocha wa Stars Etienne Ndayiragije alimuita kwenye kikosi chake kuchukua nafasi ya Jonas Mkude pale 'alipozingua' kabla Corona haijapelekea michuano ya CHAN kusitishwa
Kwa aina ya mfumo ambao Yanga wanacheza sasa, Humud anaweza kufaa zaidi pengine kuliko Tshishimbi ambaye huwa ana kawaida ya kutotulia katika eneo lake
Humud hana vitu vingi sana na pengine ndio maana mashabiki wengine wanambeza, lakini ni mchezaji ambaye akipewa kazi anaifanya ipasavyo
Nakumbuka Yanga ilipocheza na Mtibwa Sugar, Humud alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuweza kumdhibiti Morrison, pengine ndio mchezaji ambaye Morrison anaweza kumtaja kuwa alimsumbua
Huyu ni mchezaji sahihi kusimama na Fei Toto, kwani uwepo wake utampa Fei Toto Uhuru wa kuichezesha timu
Ndio, Humud ana uwezo mkubwa zaidi linapokuja suala la kukaba, hapa anaweza hata kumzidi Tshishimbi
Ni mchezaji ambaye hana papara, sio muoga na ana uzoefu wa mikikimikiki ya mechi kubwa
Tanzania imejaliwa kuwa na wachezaji wengi sana wenye vipaji, bahati mbaya huwa hawaaminiwa lakini unakuta kazi wanayofanya wakati mwingine ni zaidi ya hata wachezaji wa kigeni wanaokuja kulipwa Mamilioni
Hii ni changamoto hata kwa Yanga, pengine kuna ulazima wa kurudisha kitengo cha 'scouting' ya wachezaji ambacho kinaweza kusimamiwa na wachezaji wa zamani
0 Comments