Ndani ya kikosi cha Simba cha sasa kuna mchezaji mmoja tu ambaye pengine ndiye anayeifahamu kwa undani zaidi historia na heshima ya klabu hiyo kuliko mchezaji mwingine
Ndio, Jonas Mkude ndiye mchezaji aliyedumu kwenye kikosi cha Simba kwa muda mrefu zaidi kulinganisha na wachezaji wengine
Mkude yuko Simba kwa miaka kumi sasa. Ni nadra sana kwa wachezaji wa Tanzania kudumu kwenye klabu moja kwa muda mrefu
Historia ya Mkude na klabu ya Simba inaanzia wakati akicheza timu ya vijana, wakati huo ikinolewa na Selemani Matola mkongwe mwingine aliyecheza Simba kwa mafanikio sasa akiwa kocha Msaidizi
Ni Matola aliyebaini kipaji cha Mkude na kumjumuisha moja kwa moja kwenye kikosi chake cha vijana wa Simba na baadae kumpeleka kikosi cha kwanza
"Nakumbuka nilimuona Jonas Mkude kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya Rolling Stone yaliyofanyika Arusha nikiwa mimi na Patrick Rweyemamu (meneja wa sasa Simba) tuliona ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na angeweza kutusaidia kwenye mashindano ya vijana kwa hiyo tulimchukua na kuungana naye kwenye timu yetu ya Simba B," amesema Matola
"Tulifurahi alikuwa mchezaji muhimu kwenye timu yetu na aliisaidia sana, tuulishi naye kwenye timu ya vijana kwa miaka mitatu kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa"
"Nakumbuka kocha Patrick Phiri ndiye alimchukua baadaye kocha Phiri aliondoka timu ikawa haina kocha ikabidi mimi nichukuliwe kutoka timu ya vijana nikaenda kusaidia timu ya wakubwa kwa muda kwa hiyo tukakutana tena na Mkude"
"Tangu alivyopandishwa alikuwa bado hajaanza kucheza, mimi ndio nilikuwa mwalimu wa kwanza kumpa nafasi Mkude kwenye timu ya wakubwa. Ilikuwa Simba vs Moro United baada ya Mwinyi Kazimoto kuumia"
"Alivyoingia alionesha uwezo mkubwa sana na hapo ndipo ilianza safari ya Mkude kuchukua nafasi kwenye timu ya wakubwa hadi leo. Juhudi na uwezo ndio vinamfanya adumu hadi leo, amekuwa mchezaji muhimu ambaye kacheza kwa muda mrefu katika kipindi hiki"
0 Comments