Ujio wa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, umebadilisha utaratibu wa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, tofauti na ilivyozoeleka ili kuipa hadhi ya kimataifa.
Mchezo huo wa pili wa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unazikutanisha timu hizo kongwe, ikiwa ni baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Yusuf Singo, alisema siku ya mchezo huo kutakuwa na mabadiliko katika maeneo mbalimbali hadi jinsi ya kuingia uwanjani.
Singo alisema wamefanya hivyo ili kuimarisha usalama, pamoja na kulipa hadhi pambano hilo kutokana na ugeni unaoongozwa na Rais wa CAF.Alisema kutakuwa na utaratibi mpya wa eneo la VVIP kiasi kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kukaa sehemu bila kuwa na kadi maalum ya mwaliko.
Singo alisema kumekuwa na mazoea ya kukaa eneo hilo hata watu wasiohusika na kulifanya lishuke hadhi yake kwa sababu watu wanajaa zaidi ya idadi inayotakiwa.
“Watu wamekuwa wakijazana sana VVIP, tunapunguza msongamano huo kuanzia mechi ya Yanga na Simba, kutakuwa na kadi za mwaliko, kama mtu hajapata, asijaribu kulisogelea, atafute utaratibu mwingine.
“Kadi zinazotolewa zitakuwa na jina la mtu husika na endapo hatakuja kwenye mechi na kumpa mtu mwingine, hataruhusiwa, kadi ni ya mtu mmoja hakuna kuongeza.
“Lile eneo lina hadhi yake na idadi ya watu wanaotakiwa kukaa, lakini kwa sasa linaonekana kuzoeleka, inafika kipindi watu wengi hadi kukosa viti na hata sambusa zinazoandaliwa, tunagombea,” alisema Singo.
Alieleza kuwa ukaguzi wa watu wanaokwenda kukaa eneo hilo utaanizia chini, tofauti na awali na magari yataingia yenye kadi.Singo alifafanua kuwa barabarainayotokea Chuo cha Duse, itafungwa na magari yametengewa eneo maalum la kupaki ambalo ni ofisi za zamani za Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Naye Ofisa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (C.E.O), Almasi Kasongo, alisema wamejipanga vizuri kila eneo na anatarajia kuona Watanzania wanadumisha utamaduni wa kujaza uwanja.
Alisema anataka kuona watu wengi kwa sababu Ahmad Ahmad ameomba kuja Tanzania baada ya kuvutiwa na mashabiki wa Yanga na Simba wanavyojaza uwanja.
“Rais wa CAF amekuja katika mchezo kutokana na matukio aliyoshudia katika mchezo uliopita wa utani, hamasa na tamaduni za watani wa jadi na kuomba kuja kuona mechi hiyo,” alisema Kasongo.
Alisema kikao cha mechi kitafanyika siku moja kabla na si siku ya mchezo kama ilivyozoeleka, lakini vikosi vitawasilishwa kwa utaratibu wa kawaida
0 Comments