BETI NASI UTAJIRIKE

SIMBA YAPEWA ONYO KALI KOCHA WA AZAM AKIPIGWA FAINI


Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imemtoza faini ya Sh. 500,000 kocha Mkuu wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba kwa kosa la kugoma kuzungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya mechi dhidi ya Simba SC Machi 4, mwaka huu Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam

Taarifa ya Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo leo imesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa katika kikao cha TPLB juzi Jijini Dar es Salaam kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.


Cioaba aliyeonekana kutopendezewa na maamuzi ya marefa katika mchezo huo ambao timu yak eilichapwa 3-2 na Simba SC, ameadhibiwa kwa kuzingatia Kanuni namba 41 (12) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.


Simba nayo imepewa onyo kali baada ya kuchelewa kufika Saa 12:45 badala ya saa 12:00 katika mchezo huo – na onyo lao kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Kocha Msaidizi wa Polisi Tanzania, Ally Mtuli anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kumshambulia mwamuzi msaidizi Neema Mwambashi na kumtolea matusi ya nguoni kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC walioshinda 2-1 Machi 4 pia Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.


Wachezaji Seif Ng’ingo wa Lipuli FC na Abubakar Hashim wa Ndanda wamepigwa Faini ya kiasi cha Sh.500,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kufanya vitendo vyenye kuashiria imani za ushirikina na uchawi hadharani katika mechi baina ya timu zao iliyomalizika kw asare ya 3-3 Machi 4 Uwanja wa Samora mjini Iringa. 


Adhabu hii imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 38(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.


Klabu ya Dodoma FC imepigwa Faini ya Sh.500,000 kwa kosa la kutokufungua mlango rasmi katika uwanja wao wa nyumbani hali iliyosababisha wachezaji na viongozi wa Pan Afican kutumia mlango usio  rasmi wa kuingia Uwanjani Machi 1, mwaka Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakiibuka na ushindi wa 4-1.


Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Klabu


Nayo Geita FC imepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kutoingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo muda wa mapumziko wakitoa sare ya 1-1 na Arusha FC Machi 7, mwaka huu Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. 
Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi daraja la kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.


Nayo Dodoma FC imepigwa faini ya Sh. Milioni 1 kwa kosa la kutokufungua mlango rasmi Uwanja wao wa nyumbani hali iliyosababisha wachezaji na viongozi wa African Lyon kutumia mlango usio rasmi wa kuingia uwanjani Machi 8 wakiibuka na ushindi wa 2-1 Uwanja wa Jamhuri.


Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi daraja la kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.


Klabu ya Usalama  FC imepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la washabiki wake Kufanya vurugu na kumrushia jiwe mwamuzi wa mchezo Jackson Samwel wakitoa sare ya 1-1 na Kitayosce FC Machi 8 Uwanja wa Singe Sekondari mkoani Manyara. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.


Viongozi wa Klabu ya Mtwivila FC, Meneja wa Timu Omary Albert, Katibu wa Timu Oscar Mkusa, Kocha Mkuu Petro Mlope Kwa pamoja wanapelekwa kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kosa la udanganyifu wa Leseni ya mchezaji Christopher Rashid Kidava katika Mechi iliyochezwa Februari 29, mwaka huu wakitoa sare ya 0-0 Tukuyu Stars Uwanja wa Mkwawa Mkoani Iringa.


Vilevile Klabu ya Mtwivila FC imepoteza Mchezo huo kwa kosa la kumchezesha Mchezaji ambaye hajasajiliwa. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(23) ya Ligi daraja la Pili kuhusu udhibiti wa Klabu.
Hivyo Klabu ya Tukuyu Star FC imepewa Ushindi wa Pointi tatu na Magoli Matatu kwa uzingativu wa kanuni ya 14(36) ya Ligi daraja la pili Kuhusu taratibu za Mchezo.



Post a Comment

0 Comments