BETI NASI UTAJIRIKE

TUHUMA ZA KUPELEKWA SIMBA B ZAJIBIWA NA IBRAHIM AJIB



Siku chache tangu Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck kumtaja Ibrahim Ajibu kama mmoja ya wachezaji wasiojituma mazoezi ndio maana ameshindwa kumtumia kama ilivyo kwa Shiza Kichuya, kiungo mshambuliaji huyo amemgomea Mbelgiji huyo na kujitetea.

Hivi karibuni Sven akisema kuwa, wachezaji wanaopata nafasi ya kucheza katika kikosi chake ni wale wanaojituma na kuonyesha nia ya kucheza mazoezini, japo kuna wakati anawapanga kutokana na hitaji la benchi la ufundi.

"Kama Ajibu na Kichuya hawapo mara kwa mara katika mechi zetu za Ligi Kuu kuna tatizo, ni kwamba wenzao wanafanya vizuri kuliko wao, hakuna jambo jingine zaidi ya hilo,”

alikaririwa Sven, lakini Ajibu jana alidai kushangazwa na kauli hiyo
Nyota huyo aliyerejea Msimbazi msimu huu akitokea Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili, alisema madai kwamba huwa hajitumi kwake yamemshangaza kwa vile anapambana kwa kiwango kikubwa na kutimiza kila analoelekezwa na makocha wake kwa nia ya kuwepo katika katika kikosi cha kwanza.

Ajibu alisema kwa yeyote aliyebahatika kumuona mazoezini atajua anachokimaanisha kwani amekuwa akijituma na hata akipewa nafasi ya kucheza bado amekuwa na msaada kwa timu na hajui ni wapi anafeli kiasi cha kushindwa kuaminika kwa Sven.

"Nafahamu kikosi chetu kina nyota wazuri katika kila nafasi jambo linaloongeza ushindani katika kila idara, ila kwa jinsi ninavyofanya mazoezi, huwa nahisi kuumwa kwa kushindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye ligi na mashindano mingine wakati nipo fiti kabisa," alisema Ajibu.

Ajibu alisema kinachomuuma zaidi ni kwamba, usajili wake ni moja ya sajili zilizotumia fedha nyingi, hivyo anaposhindwa kuitumikia timu anaona ni kama anaiibia Simba, japo anasisitiza mwamuzi wa mwisho wa nani acheze ni kocha Sven na jopo lake la ufundi.

"Unajua nimesajiliwa Simba nikiwa na rekodi nzuri jambo ambalo kila shabiki wa timu hii anatamani kuona nafanya au zaidi, kwa maana hiyo nikishindwa kufikia napata maumivu makali kwangu kwani hata pale ambapo napata nafasi huwa naitendea haki,” alisema Ajibu na kuongeza;

"Angalia mechi dhidi ya Polisi Tanzania kuingia kwangu kulibadili mchezo mzima, tulikuwa nyuma lakini niliifungia timu bao la ushindi, katika mechi ya JKT Tanzania nilianza kikosi cha kwanza lakini tangu hapo nimekuwa nikiishia benchi au jukwaani."

Ajibu alisema hajakata tamaa licha ya kukosa kwake nafasi kikosini na anatumia muda mwingi kufanya mazoezi binafsi ili kuhakikisha anatumika, huku akiwapongeza wenzake kwa kujitoa kuisaidia Simba kupata ushindi kwenye mechi zao kwani inampunguzia machungu.

Katika msimu uliopita akiwa Yanga, Ajibu kama nahodha wa Yanga alifunga mabao saba na kuasisti mengine 14 kabla ya Simba kuamua kumrejesha kwenye usajili uliokuwa gumzo.
Kushindwa kung’ara kwake kwa sasa kumemfanya Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula, kumchambua akidai Ajibu ni mchezaji mzuri ila anahitaji kufundishwa na kocha anayemfahamu kwa aina yake ya maisha ilivyo anaonekana sio mchezaji aliye siriazi ila anacheza.

"Ukimuangalia kama hayupo siriazi, pia ukiachana na hilo, Ajibu yupo katika timu yenye ushindani mkubwa wa kuwania namba, jambo linalofanya akiwapo ama la hakuna anayeshtuka," alisema.

Naye nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema Ajibu ni mchezaji mzuri lakini kila kocha huwa anatoa nafasi kulingana na juhudi mazoezini.

Post a Comment

0 Comments