BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: YANGA YAENDELEA KUKIWASHA,MOLINGA NA SIBOMANA KAMA KAWAIDA YAO


Yanga SC imefanikiwa kuichapa Mbao FC mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.Ushindi huo unaifanya Yanga SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Luc Eymael anayesaidiwa na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa ifikishe pointi 47 baada ya kucheza mechi 24 na kupanda hadi nafasi ya tatu, sasa ikizidiwa pointi moja na Azam FC ambayo hata hivyo imecheza mechi moja zaidi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomari Lawi kutoka Kigoma, aliyesaidiwa na Abdulaziz Ally wa Arusha na Hamdani Said wa Mtwara, Yanga ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0.


Bao hilo limefungwa na mshambuliaji wake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga Ndama ‘Falcao’ kwa penalti dakika ya 22 kufuatia kiungo Fundi, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuangushwa kwenye boksi na beki Hussein Abdallah.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili, kocha wa Yanga SC, Luc Eymael alifanya mabadiliko akimuingiza mshambuliaji mpya, Tariq Seif Kiakala kwenda kuchukua nafas ya Molinga ambaye alikwenda kutoa mchango katika bao la pili. 
Kiakala alipokea pasi ya mtokea benchi mwingine Mapinduzi Balama akatia krosi fupi ya chinichini Mrisho Ngassa akairuka kuwazuga mabeki wa Mbao FC na kumkuta mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Sibomana aliyefunga bao la pili dakika ya 81.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC wanakwenda kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wa jadi, SImba SC Jumapili hapo hapo Uwanja wa Taifa kuanzia Saa 11:00 jioni.


Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikalo, Juma Abdul, Adeyum Ahmed, Lamine Moro/Ally Mtoni dk82, Kelvin Yondani, Papy Kabamba Tshishimbi, Mohamed Issa/Balama Mapinduzi dk71, Feisal Salum, David Molinga/Tariq Seif dk63, Mrisho Ngassa na Patrick Sibomana.


Mbao FC; Rahim Abdallah, Aboulrahman Said, Makiada Makolo, Hussein Abdallah, Babilas Chitembe/Emmanueli Charles dk46, Rajabu Rashid, Mussa Gabi, Omary Wayne/Dasco Frank dk79, Ndaki Robert/Jordan John dk69, Waziri Junior na Herbert Lukindo.

Post a Comment

0 Comments