BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: SIMBA NI MWENDO WA KUTOA VIPIGO , YANGA JIANDAENI


Simba SC wameendelea kudhihirisha ubora wao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC usiku wa leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck anayesaidiwa na mzawa Suleiman Matola inafikisha pointi 68 baada ya kucheza mechi 26, sasa ikiizidi pointi 20 Azam FC inayofuatia nafasi ya pili. 


Nyota aliyeihakikishia Azam FC kuondoka na pointi zote tatu hii leo ni mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere ‘MK 14’ aliyefunga bao la ushindi dakika za mwishoni baada ya kutokea benchi kipindi cha pili.


Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Mbaraka Hailey, wote wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Lakini wekundu wa Msimbazi walilazimika kutokea nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao la dakika ya nne la kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe, Never Tigere.

Beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni aliisawazishia Simba SC dakika ya nane, kabla ya kiungo mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deogratius Kanda kufunga bao la pili dakika ya 15, wote wakimalizia pasi za kiungo Mzambia, Clatous Chama.

Kipindi cha pili Azam FC inayofundishwa na kocha Mromania, Aristica Cioaba walirudi na mipango mizuri na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 49 akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda. Hata hivyo, Kagere aliyengia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kanda akaifungia Simba bao la tatu dakika 70 akimalizia krosi ya Shomari Salum Kapombe kutoka kulia.


Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akauwahi mpira uliotemwa na kipa Aishi Salum Manula kufuatia shuti la umbali wa mita 30 la mshambuliaji Muivory Coast, Rchard Ella D’jodi na kuukwamisha nyavuni dakika ya 82, lakini refa msaidizi namba moja, Hellen Mduma akakataa akisema mfungaji alikuwa ameotea.
Wachezaji wa Azam FC walijaribu kumshawishi Hellen akubali bao hilo, lakini wakaambulia adhabu baada ya Iddi Nado kuonyeshwa kadi ya njano.


Simba SC inakwenda kambini kujiandaa na mchezo mwingine mgumu wa Ligi Kuu dhidi ya mahasimu wao wa jad, Yanga Jumapili hapo hapo Uwanja wa Taifa.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nicholas Wadada, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohamed, Bryson Raphael/Frank Domayo dk69, Idd Suleiman ‘Nado’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Chilunda/Richard D’jodi dk76, Obrey Chirwa na Never Tigere/Idd Kipagwile dk76.

Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda/Meddie Kagere dk62, Clatous Chama, John Bocco, Luis Miquissone/Sharaf Eldin Shiboub dk83 na Francis Kahata.

Post a Comment

0 Comments