BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: MEDDIE KAGERE BABA LAO APIGA 4 SIMBA IKIICHAKAZA SINGIDA



Simba SC wamepoza machungu ya kufungwa na watani wa jadi, Yanga kwa kuichapa SIngida United 8-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Simba SC iliyo chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ifikishe pointi 71 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 17 zaidi ya Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili.


Hali inazidi kuwa mbaya kwa mbaya Singida United iliyo chini ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswanzurimo, kwani baada ya kipigo cha leo kwenye mchezo uliochezeshwa na refa Ludovic Charles wa Mwanza aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Credo Mbuya wa Mbeya – inabaki na pointi zake  12 za mechi 28 mkiani


Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere manne dakika ya pili, 26, 41 na 71, kiungo Deogratius Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mawili dakika ya 13 na 18, mshambuliaji na Nahodha John Bocco dakika ya 19 na kiungo Msudan, Sharaf Eldin Shiboub dakika ya 60.
Singida United ilimaliza pungufu baada ya kiungo wake mkongwe, Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 57 kufuatia kumpiga kisukusuku kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula wakati wanasubiri mpira wa kona.


Mechi iliyopita Simba SC ilifungwa 1-0 na watani wao jadi, Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la kiungo Mghana, Bernard Morrison dakika ya 44 – hivyo ushindi wa kishindo leo unaweza kuwasahaulisha kipigo cha Machi 8.


Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, bao pekee la Ismail Azizi dakika ya 80 akimalizia pasi ya Adily Buha limetosha kuipa Tanzania Prisons ushindi wa 1-0 dhidi ya Alliance FC ya Mwanza leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.


Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe/Gardiel Michael dk46, Mohamed Hussen ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Pascal Wawa, Jonas Mkude/Sharaf Eldin Shiboub dk46, Deo Kanda, Luis Miquissone, Medie Kagere, John Bocco/Gerson Fraga dk51 na Hassan Dilunga.


Singida United; Owen Chaima/Geogfrey Mkumbo dk46, Geogre Wawa, Haji Mwinyi, Meshak Kibona/Jonathan Daka dk46, Tumba Sued, Cleophace Sospeter, Geogre Sangija, Haruna Moshi, Steven Sey, Seiri Arigumelo/ David Nartey dk21 na Said Mtikila.

Post a Comment

0 Comments