BETI NASI UTAJIRIKE

WADAU WATOA MAONI LIGI KUCHEZWA BILA MASHABIKI
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amesema uamuzi uliotangazwa na Bodi ya Ligi wa kuruhusu ligi kuendelea baada ya siku 30 lakini wakizuia mashabiki viwanjani kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona si sahihi na si suluhisho kwa tishio lililopo la ugonjwa huo ambao unaisumbua dunia kwa sasa.

Mwakalebela amesema TFF na vyombo vyake inapaswa kuwa na subira kwa sababu endapo virusi vya corona vitaendelea kuwapo, itakuwa vigumu kudhibiti mkusanyiko wa mashabiki kwenye 'vibanda umiza' ambavyo vimeenea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

"Bado haitakuwa suluhisho, mkusanyiko wa watu utaendelea kuwapo, hatuna uwezo wa kudhibiti katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yatakusanya mashabiki, ni bora tusubiri janga limalizike, huko duniani (nchi zilizoendelea), wameona haina tija, iweje sisi tucheze," Mwakalebela alisema.

Naye mchambuzi maarufu wa soka na nyota wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars), Ally Mayayi alisema mechi za Ligi Kuu Bara kuchezwa bila mashabiki zitakuwa na madhara kiuchumi kwa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo.

Mayayi alisema klabu zote zinategemea kujiendesha kwa kutegemea mapato ya milangoni, hivyo kuchukua uamuzi huo kutazifanya timu kuyumba.

"Kwanza ligi kusimama kwa siku 30 kuna madhara makubwa sana, kutafanya viwango vya wachezaji kushuka, upo uwezekano mkubwa wachezaji wakarejea wakiwa hawako fiti, hii italeta matatizo na kuzalisha matokeo yasiyotarajiwa," alisema Mayayi.

Aliongeza kusimama kwa ligi kutazalisha madeni ambayo klabu hazikujiandaa kutokana na kuzuka kwa janga hilo ambalo limesimamisha ligi na mashindano mbalimbali duniani.

"Hata bajeti zilizopo kwa klabu imekuwa haitoshi, ligi itakapokuwa imesimama ni wazi kutakuwa na gharama ambazo zitakuwapo, kuna klabu zimekuwa zinapata tabu hata ya usafiri na malazi, klabu zitazalisha madeni mapya, malimbikizo ya posho kama ambayo tumekuwa tukisikia malalamiko ya kudai mishahara," Mayayi aliongeza.

Post a Comment

0 Comments