CEO WA SIMBA ATAJA MBINU MPYA WANAZOTUMIA KUSAJILI



Kuelekea msimu ujao na kukabiliana na ushindani katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Simba ya jijini Dar es Salaam umesema hautafanya usajili wa kukurupuka au 'mihemko'

Simba yenye pointi 71, ndio mabingwa watetezi na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wamepoteza mechi tatu kati ya michezo 28 waliyocheza.Kimahesabu ni mabingwa wanaosubiri kutangazwa pamoja na kuwa wanahitaji kushinda mechi tano kati ya 10 zilizosalia. Kwa ushindani ulivyo, haitarajiwi washindani wake Yanga na Azam Fc kushinda mechi zao zote zilizosalia hivyo uongozi wao wa zaidi ya alama 17 unawaweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema wamejiandaa kusajili wachezaji wenye viwango vya juu kutoka katika ligi zenye mafanikio hapa barani Afrika na kwa kutumia kampuni zenye uzoefu na kazi hiyo.

Senzo alisema wanahitaji wachezaji ambao wana uwezo na uzoefu wa kupambana katika mashindano ya kimataifa na kamwe Simba haiangalii mechi za Ligi Kuu Bara au michuano ya Kombe la FA pekee.

"Katika suala la usajili tumeshaanza skauti katika maeneo mengi hapa barani Afrika ili kupata wachezaji bora na imara, pengine tutafanya usajili mzuri kuliko misimu yote kwa sababu tutaangalia vigezo vingi kulingana na mahitaji yetu," alisema Senzo.

Senzo amesema katika kukamilisha mchakato wa kusajili wachezaji wapya, klabu itazingatia zaidi ripoti ambayo itaeleza wazi ubora na upungufu alionao mchezaji husika kabla ya kufanya uamuzi wa kumpa mkataba.
Kiongozi huyo ameweka wazi katika kuendeleza vipaji kwa faida ya nchi, Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck ametoa baraka ya kutolewa kwa mkopo kwa wachezaji ambao wanakosa namba katika kikosi chake au kuruhusiwa kujiunga na klabu nyingine kwa wale waliomaliza mikataba yao ndani ya Simba.
"Katika ligi ya hapa ndani tunaweza kusajili wachezaji kama wawili, na waliobakia tutaangalia kwenye nchi nyingine za Afrika, ambazo zimeendelea kisoka, hii itatusaidia kutimiza malengo yetu"

Post a Comment

0 Comments