Mabingwa wa nchi Simba leo wanatupa karata muhimu uwanja wa Taifa watakapoikabili Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ambao utapigwa kuanzia saa moja usiku
Ugumu wa mchezo huo unatokana na ubora wa timu ya Azam kwani ukiondoa Simba pengine Azam Fc na kidogo Yanga ndio zinazofuata kwa ubora miongoni mwa timu zinazoshiriki ligi kuu
Lakini pia msimu huu tayari Azam Fc imeshakubali vipigo viwili kutoka kwa Simba
Kipigo cha kwanza kilikuwa cha mabao 4-2 mchezo wa Ngao ya Jamii kisha kupigwa bao 1-0 mchezo wa duru ya kwanza ligi kuu
Hivyo ni wazi wataingia kwenye mchezo huo kujaribu kujihami na kipigi cha tatu mfululizo
Hata hivyo wanakutana na Simba wakati mbaya, kwani mabingwa hao watetezi wamerejea kwenye ubora wao
Simba imeshinda mechi tano mfululizo kwenye ligi na sasa inapiga hesabu za kutwaa ubingwa mapema.Ushindi katika mechi nane kati ya 13 zilizobaki, utaihakikishia Simba kutwaa ubingwa
Mkufunzi wa timu hiyo Sven Vandenbroeck amesema ushindi katika mechi ya leo na inayofuata dhidi ya Yanga ndio matokeo muhimu zaidi kwao kuelekea kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo
0 Comments