Yanga SC wameendelea kusuasua baada ya kulazimishwa sare ya tatu mfululizo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia kufungana 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Ikumbukwe, Yanga SC ilitoa sare za 0-0 na Mbeya City na 1-1 na Tanzania Prisons, zote za Mbeya kwenye mechi zake mbili zilizopita Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Na sare ya leo inamaanisha wameshindwa kuifunga Polisi msimu huu, kwani hata mechi ya kwanza walitoka sare ya 3-3 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam tena Yanga wakitoka nyuma 3-0 kipindi cha kwanza.
Katika mchezo wa leo, Yanga SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata leo, mfungaji Tariq Seif Kiakala dakika ya 41 akimalizia pasi ya kiungo Mghana, Benard Morison.
Lakini Polisi Tanzania wakasawazisha bao hilo dakika ya 67 likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Matheo Anthony Simon kwa kichwa akimalizia krosi ya Suxtus Sabilo, ambalo hata hivyo lilikataliwa.
Refa Abel William alimfuata msaidizi wake namba moja, Martin Mwaliaje kushauriana naye na wakalikataa bao hilo.akini Polisi Tanzania hawakukata tamaa na kwa kutumia makosa ya aina ile ile ya safu ya ulinzi ya Yanga, wakafanikiwa kupata bao lingine dakika tatu baadaye, mfungaji Sixtus Sabilo akimalizia pasi ya Marcel Kaheza dakika ya 71.
Sare hii inaifanya Yanga SC ifikishe pointi 40 katika mchezo wa 21, ingawa inabaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 44 na Simba SC wenye pointi 59 baada ya wote kucheza mechi 22.
Kikosi cha Polisi Tanzania kilikuwa; Mohamed Yussuf, William Lucian, Yassin Mustapha, Iddy Mobby, Mohammed Kassim, Pato Ngonyani, Jimmy Shoji, Baraka Majogoro/Mohamed Mkopi dk62, Matheo Anthony, Marcel Kaheza na Sixtus Sabilo.
Yanga SC; Farouk Shikharo, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Kelvin Yondan, Lamine Moro, Pappy Kabamba Tshishimbi, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima/Abdulaziz Makame dk85, Tariq Seif/Yikpe Gislain dk64, Mapinduzi Balama/Deus Kaseke dk78 na Benard Morrison.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, JKT Tanzania imetoa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa Uhuru, huku Namungo FC ikiichapa 2-1 KMC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi. Mabao ya Namungo yamefungwa na Bigirimana Blaise dakika ya 12 na 65 huku la KMC likifungwa na James Msuva dakika ya 84.
Pamoja na kutangulia kwa bao la Mudathir Said dakika ya 50, lakini Coastal Union leo imechapwa 2-1 nyumbani na Ruvu Shooting ambayo ilitokea nyuma kwa mabao ya Saadat Mohamed dakika ya 77 na Graham Naftari dakika ya 90 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Mbeya City ikaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao yake yakifungwa na Seleman Ibrahim dakika ya 11 na Peter Mapunda dakika ya 86, bao pekee la wageni likifungwa na kipa Deogratias Munishi dakika ya 90 na ushei, yote kwa penalti.
Nayo Mbao FC ikaibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Singida United, mabao yake yakifungwa na Mussa Haji dakika ya 26, Herbeth Lukindo dakika ya 45 na Jordan John dakika ya 66 huku la wageni likifungwa na Daudi Mbweni dakika ya 90.
0 Comments