BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: SIMBA YAENDELEA KUTOA VIPIGO LIGI KUU

Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Kagera Sugar 1-0 usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.


Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 59 katika mchezo wa 23, ikitanua uongozi wake kwa pointi 15 zaidi ya Azam FC wanaofuatia ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi na kesho watamenyana na Ndanda FC mjini Mtwara.  
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro aliyesaidiwa na Arnold Bugado wa Tanga na Rashid Zongo wa Iringa, bao pekee la Simba SC limefungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere kwa penalti dakika ya 60.


Penalti hiyo ilitolewa na Saanya baada ya mshambuliaji na Nahodha wa Simba SC, John Raphael Bocco kuangushwa na kipa Benedictor Tinocco kwenye boksi.
Ushindi wa leo unamaanisha Simba SC imejivua kabisa unyonge uliodumu kwa misimu miwili iliyopita mbele ya Kagera Sugar kutokana na kufungwa mechi zote nne – baada ya wao bao kuwafunga nyumbani na ugenini wana Bukoba hao. 
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, JKT Tanzania imetoa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa Uhuru, huku Namungo FC ikiichapa 2-1 KMC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi. Mabao ya Namungo yamefungwa na Bigirimana Blaise dakika ya 12 na 65 huku la KMC likifungwa na James Msuva dakika ya 84.
Pamoja na kutangulia kwa bao la Mudathir Said dakika ya 50, lakini Coastal Union leo imechapwa 2-1 nyumbani na Ruvu Shooting ambayo ilitokea nyuma kwa mabao ya Saadat Mohamed dakika ya 77 na Graham Naftari dakika ya 90 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Mbeya City ikaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao yake yakifungwa na Seleman Ibrahim dakika ya 11 na Peter Mapunda dakika ya 86, bao pekee la wageni likifungwa na kipa Deogratias Munishi dakika ya 90 na ushei, yote kwa penalti.
Nayo Mbao FC ikaibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Singida United, mabao yake yakifungwa na Mussa Haji dakika ya 26, Herbeth Lukindo dakika ya 45 na Jordan John dakika ya 66 huku la wageni likifungwa na Daudi Mbweni dakika ya 90.
Nao Yanga SC wakalazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika mjini Moshi Kilimanjaro. Yanga SC walitangulia kwa bao la Tariq Seif Kiakala dakika ya 41, kabla ya Polisi Tanzania kusawazisha kupitia kwa Sixtus Sabilo dakika ya 71.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone/Hassan Dilunga dk79, Clatous Chama, John Bocco/Sharaf Shiboub dk84, Meddie Kagere na Francis Kahata.

Kagera Sugar; Beneditc Tinocco, Ally Shomary, David Luhende, Erick Kyaruzi, Juma Nyosso, Zawadi Mauya, Yusuph Mhilu/Peter Mwalyanzi dk67, Abdallah Seseme, Kelvin Sabato/Awesu Awesu dk52, Nassor Kapama na Ally Ramadhani.

Post a Comment

0 Comments