BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: SIMBA WAIBOMOA MTIBWA SUGAR BILA HURUMA

Simba SC wamezinduka na kuichapa Mtibwa Sugar 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri Jijini Morogoro.Kwa ushindi huo, Simba SC iliyo chini ya Kocha Mkuu, Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck anayesaidiwa na mzalendo, Suleiman Matola, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’ na kocha wa Fiziki, Mtunisia, Adel Zrane inafikisha pointi 53 katika mchezo wa 20 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 12 zaidi ya Azam FC.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Abdallah Mwinyimkuu wa Singida aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono wa Dar es Salaam – hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.


Ni bao lililofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco dakika ya 45 akinufaika na uzembe wa mabeki wa Mtibwa Sugar baada ya pasi ya mshambuliaji mwenza, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.

Kipindi cha Simba SC, mabingwa mara mbili mfululizo na mara 20 jumla wakishika nafasi ya pili kutwaa taji hilo mara nyingi nyuma ya mahasimu wao wa jadi, Yanga waliotwaa mara saba zaidi – walirejea na moto ule ule na kufanikiwa kupata bao la pili dakika mbili tu tangu mchezo uanze tena.
Bao hilo lilifungwa na Nahodha wake Msaidizi, beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya 47 kwa shuti la kiufundi baada ya pasi ndefu ya kiungo Jonas Gerlad Mkude.

Bao hilo liliwavuruga kabisa Mtibwa Sugar na haikuwa ajabau wakaongezwa lingine, wakifungwa na mchezaji wao zamani, kiungo Hassan Dilunga dakika ya 59 akimalizia pasi ya Nahodha, Bocco baada ya gonga safi za Wekundu wa Msimbazi kutokea nyuma.
 
Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Shaaban Kado, Kibwana Shomari, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Job, Henry Joseph, Abdulhalim Humud, Ally Yussuf, Boban Zirintusa/Omari Hassan dk75, Stahmil Mbonde, Juma Luizio na Haroun Chanongo/Ismail Mhesa dk70.

Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe/Haruna Shamte, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco/Luis Miquissone dk78 na Francis Kahata.

Mechi nyingine za Ligi Ku leo, bao pekee la Atupele Green dakika ya 63 lilitosha kuwapa Biashara United ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.

Na Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Azam FC ikaibuka na ushindi wa 1-0 pia dhidi ya Polisi Tanzania ya Kilimanjaro, bao pekee la kiungo Mudathir Yahya dakika ya 48.

Uwanja wa Liti mkoani Singida, bao pekee la Zingamasebo Steven dakika ya 68 likaipa Namungo FC ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji, Singida United.

Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, mabao ya Samuel John dakika ya 69 na Omary Khamis dakika ya 89 yakaipa ushindi wa 2-0 Ndanda FC dhidi ya wenyeji, Mwadui FC.

Kagera Sugar wakakubali kichapo 2-1 nyumbani mbele ya Alliance FC ya Mwanza Uwanja wa Kaitaba mkoani Bukoba mabao ya wageni yakifungwa na Martin Kigi dakika ya 64 na David Richard dakika ya 90 na ushei huku bao pekee la wenyeji likifungwa Nassor Kapama dakika ya 90. 

Lipuli FC ikalazimishwa sare ya 1-1 na JKT Tanzania Uwanja wa Samora mkoani Iringa tena yenyewe ikisawazisha kupitia kwa Issah Ngoah dakika ya 17 baada ya Edson Katanga kuanza kuwafungia wageni dakika ya tano.

Post a Comment

0 Comments