BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI : FALCAO ALIVYOWAPA YANGA USHINDI DHIDI YA MTIBWA SUGAR

BAO pekee la mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga Ndama ‘Falcao’ leo limeipa Yanga SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.


Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na Mbelgiji Luc Aymael anayesaidiwa na mzawa, Charles Boniface Mkwasa, kocha wa Fiziki, Riedoh Berdien kutoka Afrika Kusini na kipa wa zamani wa klabu, Manyika Peter anayewanoa walinda milango wa timu hiyo inafikisha pointi 31 baada ya kucheza mechi 16 na kupanda nafasi ya nne.


Yanga SC inalingana na Namungo FC inayoshika nafasi ya tatu ikiwa imecheza mechi moja zaidi na kwa pamoja wanazididi pointi moja moja, Kagera Sugar, Coastal Union na Polisi Tanzania ambazo zote zimecheza mechi 18 na wanazidiwa pointi 16 na vinara, Simba SC ambao pia ndio mabingwa watetezi.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa aliyesaidiwa na Robert Luhemeja wote wa Arusha na Mohamed Mkono wa Tanga, Molinga aliye katika msimu wake wa kwanza baada ya kusajiliwa kutoka AC Lega ya kwao alifunga bao hilo dakika ya 50 akimalizia krosi ya mtokea benchi Ditram Adrian Nchimbi.

Na hiyo ilifuatia dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Mtibwa Sugar wakiidhibiti vizuri Yanga iliyokuwa inacheza kwa kushambulia.
Na sifa zaidi zimuendee kiungo mkongwe, Abduhalim Humud ‘Gaucho’ aliyemdhibiti kiungo matata wa klabu hiyo, Bernard Morrison kutoka Ghana. 

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Patrick Sibomana/Ditram Nchimbi dk46, Haruna Niyonzima, David Molinga/Yikpe Gislain dk68, Mapinduzi Balama na Bernard Morrison/Abdulaziz Makame dk85.

Mtibwa Sugar; Shaaban Kado, Kibwana Shomari, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Cassian Ponera, Henry Shindika, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, Ismail Mhesa/Juma Luizio dk56, Ally Makarani, Riphat Msuya/Haroun Chanongo dk81, Awadh Juma na Salum Kihimbwa/Omary Hassan dk73.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; bao la dakika ya 88 la Muivory Coast, Richard Ella D’jodi liliinusuru Azam FC kulala kwa Mbeya City iliyotangulia kwa bao la Abasalim Chidiebere dakika ya dakika ya tisa na kufanya sare 1-1 Uwanja wa Samora mjini Iringa. 

Na bao pekee la Jimmy Shoji dakika ya 76, likaipa Polisi Tanzania ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, wakati Tanzania Prisons imeichapa KMC 1-0, bao pekee la Jeremiah Juma dakika ya 22 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments