MASAU BWIRE AKERWA NA VIONGOZI WA PRISONS KWA TUKIO WALILOLIFANYA

Msemaji wa klabu ya Ruvu Shoting ameonekana kukerwa na viongozi wa klabu ya Prisons baada ya kuugomea mchezo wao wa jana. Timu hizo zilikuwa na mechi hapo jana lakini mchezo huo haukuchezwa huku Masau Bwire akisimulia tukio zima 


Masau Bwire ameandika hivi 

"Mchezo kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Tanzania Prisons umeahirishwa baada ya Tanzania Prisons kuugomea.Saa 8 mchana, wakati tayari Ambulance ipo uwanjani, ilitokea dharura, mgonjwa mahututi ahamishiwe Hospitali ya Lugalo kwa matibu zaidi.

Baada ya Ambulance hiyo kuondoka, ilitafutwa gari nyingine ambayo haikuwa Ambulance ili ifanye kazi kwa muda wakati huo ikitafutwa Ambulance nyingine.

Kituo cha Afya Mlandizi kilitoa Ambulance kwenda uwanjani kwa  huduma ya hapo , ilifika ikiwa imechelewa dakika 2.

Mwamuzi kwa kushauriana na Match com walikubaliana mpira uanze, Wachezaji waliingia uwanjani tayari kuanza mchezo, muda mfupi kabla refa hajaanzisha mchezo, viongozi wa Prisons waliwaambia wachezaji wao watoke uwanjani wasicheze mchezo huo.

Baada ya mwamuzi wa mchezo kuwasihi kwa muda mrefu wachezaji wa Prisons wakubali kucheza bila mafanikio, aliwaita makepteni wa timu zote mbili akawaeleza kwamba, alikuwa tayari kuanzisha mchezo, lakini kwakuwa Prisons wamegoma, amelazimika kuuahirisha, utapangiwa tarehe nyingine ya kurudiwa au vinginevyo.

Kitendo cha Prisons kugomea mchezo ule, hakikutuumiza sisi tu Ruvu Shooting, kiliwaumiza sana mashabiki wa soka waliolipa viingilio vyao kwa ajili ya kuuangalia mchezo huo.

Hivi kwa dharura kama ile, ambayo haikutarajiwa kwa muda kama huo, kama ni wewe ungefanyaje?
Iwe kwamba wewe mwenyewe au ndugu yako wa karibu, mwanao, mkeo, baba, mama au yeyote ndugu yako, yuko mahtuti, anatakiwa apelekwe kwa haraka Hospitali ya juu ili kupata tiba ambayo huenda ikaokoa uhai wa maisha yake, ukaambiwa hawezi kupelekwa kwasababu Ambulance ambayo ingempeleka ipo uwanjani kwa ajili ya kuwahudumia wachezaji watakaoumia!

Kwa akili ya kawaida, hivi kweli Ruvu Shooting, inayolelewa na taasisi kubwa kiasi kile, inaweza kukosa na kushindwa kabisa kupeleka Ambulance uwanjani wakati tunajua kwa kufanya hivyo tunapoteza pointi!."

Post a Comment

0 Comments