BETI NASI UTAJIRIKE

SIMBA KUTAMBULISHA MASHINE YAO MPYA MECHI NA MWADUI

Baada ya kuvuna pointi sita muhimu katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara huko Kanda ya Ziwa, kikosi cha Simba jana kimeingia kambini kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA, huku kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya akiwemo kati yao.


Simba inajianda na mechi ya Mwadui FC ya mkoani Shinyanga itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Jumamosi hii.

Katika mchezo huo, Simba wataingia uwanjani wakiwa na hasira za kufungwa katika mchezo wa ligi uliopigwa Uwanja wa Kambarage huko Shinyanga ambao ulimalizika kwa Mwadui kushinda bao 1-0. Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema kuwa kikosi chao kitaingia kambini leo jioni huko Ndege Beach nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Rweyemamu alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri na wachezaji wote wataingia kambini tayari kwa kuwawinda Mwadui kwa ajili ya kulipa kisasi cha kufungwa katika ligi.

Aliongeza kuwa kiungo wao wa zamani Kichuya huenda akawa katika sehemu ya wachezaji watakaoingia kambini baada ya hivi karibuni kusaini mkataba wa kuichezea Simba.

“Kesho (jana), timu yetu itaingia kambini rasmi huko Ndege Beach tulipoweka kambi ya kudumu katika msimu huu kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Mwadui.

“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa kombe hili, hivyo ni lazima timu yetu ipate matokeo mazuri ili tuendelee na mashindano hayo na mwisho wa siku tuweze kuchukua kombe hilo.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na timu yetu  na wachezaji wote wataingia kambini kujiandaa na mchezo huo, pia Kichuya huenda akawa sehemu ya wachezaji watakaoingia kambini  kama atakuwa amekamilisha baadhi ya vitu vyake kati yake na uongozi baada ya kusaini mkataba Simbva,” alisema Rweyemamu ambaye ni miongoni mwa wanachama wanaoaminika sana na uongozi wa juu wa Simba.

Post a Comment

0 Comments