BETI NASI UTAJIRIKE

RIPOTI YA MECHI: HIVI NDIVYO YANGA WALIVYOPIGWA GOLI 3-0 NA KAGERA SUGAR

 Kagera Sugar leo imewaadhibu vigogo, Yanga SC kwa kuwachapa 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru Taifa Jijini Dar es Salaam. Kwa ushindi huo, Kagera Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mecky Mexime inafikisha pointi 27 katika mchezo wa 17 na kupanda had nafas ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.


Yanga SC inayobaki na pointi zake 25 baada ya kucheza mechi 13 sasa ni ya nane, wakati Simba SC inaendelea kuongoza kwa pointi zake 35 za mechi 14, ikifuatiwa na Coastal Union yenye pointi 30 za mechi 17 na Namungo FC point 28 mechi 15. 


Mchezaji wa zamani wa Yanga kuanzia timu ya vijana, Yusuph Mhilu ndiye aliifungia Kagera Sugar bao la kwanza dakika ya 13 kwa shuti la umbali wa mita 14 akimalizia mpira aliotengewa na beki wa wapinzani, Kelvin Yondan.

Yanga ikapata pigo dakika ya 44 baada ya kiungo wake, Mohammed Issa ‘Banka’ kutolewa kwa kadi nyekundu na refa Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.


Wakati wa mapumziko, kocha mpya wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael alimfuata refa Mwinyimkuu pamoja na wasaidizi wake Nestory Livangala wa Tabora na Leonard Mkumbo wa Manyara kuwazonga. 


Na kipindi cha pili Yanga haikuonyesha kubadilika kabisa, zaidi Kagera Sugar waliimarika maradufu na kuendelea kuutawala mchezo. 
Haikuwa jambo la ajabu Ally Ramadhan alipoifungia bao la pili Kagera Sugar dakika ya 67, akimalizia pasi ya kiungo Abdallah ‘Dullah’ Seseme.Na hakika bao hilo liliwavuruga zaidi Yanga na kuacha kabisa kushambulia japo kwa kushitukiza, wakibaki katika eneo lao kuzuia ili wasiruhusu mabao zaidi.

Lakini mtokea benchi, kiungo Peter Mwalyanzi akafanikiwa kutikisa tena nyavu za ‘Watoto wa Jangwani’, akiifungia Kagera Sugar bao la tatu dakika ya 90 baada ya kazi nzuri ya beki wa zamani wa Yanga, David Luhende.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikaro, Paul Godfrey ‘Boxer’/Yikpe Gislain dk68, Adeyum Ahmed, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama/Deus Kaseke dk82, Mohamed Issa ‘Banka’, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Patrick Sibomana/Mrisho Ngassa dk55.

Kikosi cha Kagera Sugar; Benedicto Tinoco, Mwaita Gereza, David Luhende, Juma Nyosso, Erick Kyaruzi, Zawadi Mauya, Yussuf Mhilu, Abdallah Seseme, Kelvin Sabato/Peter Mwalyanzi dk77, Nassor Kapama na Frank Ikobela/Jackson Kibirige dk11/Ally Ramadhan dk54. 

Post a Comment

0 Comments