Mashabiki wa Simba walikuwa wakiimba maneno ya msemaji wao, Haji Manara kwamba wao hawapo levo moja na timu nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuishushia mvua ya mabao Alliance
Simba iliichapa Alliance 4-1, ikiwa imetangulia kufungwa kwa bao la Israel Mwenda dakika ya 25 lakini ikarejea na kupindua matokeo.Ushindi huo, umekuja siku moja baada ya mahasimu wao Yanga kuchapwa bao 1-0 na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba walisawazisha bao dakika ya 45+3 kupitia kwa Jonas Mkude akipokea pasi safi kutoka kwa Sharaf Shiboub, na hivyo kwenda mapumziko wakiwa 1-1.
Simba walirejea kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 58 kupitia kwa Medie Kagere aliyeifanyia kazi vizuri pasi kutoka kwa kiungo fundi, Clatous Chama.
Bao la tatu la Simba lilifungwa na Chama kwa faulo ya moja kwa moja akiwa nje ya 18 dakika ya 63. Simba walihitimisha karamu ya mabao kwa bao safi la Hassan Dilunga akipokea asisti ya Sharaf Shiboub dakika ya 72.
Simba waliutawala vizuri mchezo huo huku wakikosa nafasi nyingi za wazi hasa kipindi cha kwanza katika uwanja ambao ulikuwa na matope katika baadhi ya sehemu kutokana na mvua iliyonyesha kabla ya mechi.
Dilunga angeweza kufunga bao akiwa na mlinda mlango kipindi cha kwanza lakini shuti alilopiga lilipaa, Shiboub naye alipaisha mpira akiwa ndani ya 18 kipindi cha kwanza. Lakini Simba walipiga pasi nyingi na kuonyesha soka maridadi licha ya uwanja kuwa na matope baadhi ya sehemu.
Alliance nao wangeweza kuongeza bao kipindi cha pili wakati matokeo yakiwa 1-1, baada ya mchezaji wao kupiga shuti ambao Kakolanya alilipangua na kuwa kona.
Matokeo hayo ya Mnyama, yanamaanisha kuwa wamefikisha pointi 41 na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu baada ya kucheza mechi 16.
Sasa wamewaacha mahasimu wao Yanga kwa tofauti ya pointi 16 lakini Yanga wakiwa wamecheza mechi 14 wakiwa katika nafasi ya nane baada ya kujikusanyia pointi 25.
Simba pia wamewaacha kwa tofauti ya pointi tisa Azam wanaoshika nafasi ya pili lakini Azam wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema kuwa atahakikisha timu yake inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Sven ambaye ameshinda mechi tano na sare moja katika michezo sita ya ligi aliyocheza tangu atue Msimbazi, amesema: “Ushindani ni mkubwa lakini kwa jinsi tulivyojipanga, timu yangu itahakikisha inachukua ubingwa.”
0 Comments