Mshambuliaji raia wa Ghana Bernard Morrison, rasmi juzi alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam tayari kwa kujiunga na Klabu ya Yanga.
Mghana huyo alitua kwenye uwanja huo saa 2:15 asubuhi na ndege aina ya Kenya Airways na kupokelewa na Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz kabla ya kuondoka naye hapo.
Yanga imemsajili mshambuliaji huyo ikiwa ni saa chache kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa juzi Jumatano saa sita kamili usiku kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao kilichopanga kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara unaotetewa na watani wao wa jadi, Simba.
Mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege huo, Morrison alifanya ‘Exclusive Interview’ na www.amospoti.com na kusema kuwa ana furaha kubwa kujiunga na moja ya klabu kubwa Afrika amepanga kuifanyia makubwa kwa kipindi chote atakachokuwepo Yanga ikiwemo kutwaa mataji.
Morrison alisema kuwa amejiunga na Yanga kwa ajili ya kuipa makombe na siyo pesa ila anaomba sapoti kutoka kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa timu hiyo.
Alisema kuwa anajiunga na Yanga akiwa tayari anazijua klabu pinzani ambazo ni Simba na Azam FC akiamini akiwa na klabu yake hiyo mpya atahakikisha anaipambania ili kuhakikisha kila atakapokutana nazo wanapata ushindi.
Aliongeza kuwa hatawaangusha mashabiki wa Yanga kwa kipindi chote atakachokuwepo uwanjani huku akiamini uzoefu mkubwa alionao wa kuzichezea klabu kubwa Afrika ambazo ni DC Motema Pembe ya DRC 2018, Orlando Pirates (Afrika Kusini) 2016-2018, AS Vita (DRC) 2015-2016, Ashanti Gold FC 2013-2015 na Hearts of Lions 2010-2013 zote za Ghana.
“Nina furaha kubwa kujiunga na klabu kubwa Afrika niliyojiunga nayo kwenye msimu huu, na malengo yangu ni kuona timu yangu inapata mafanikio kutokana na uwepo wangu na kikubwa ni kuhakikisha tunachukua makombe.
“Hilo linawezekana kabisa, kwani kama mimi mshambuliaji nitahakikisha ninatimiza majukumu yangu ya kutumia kila nafasi nitakayoipata katika kufunga mabao na uzuri uwezo huo wa kufunga mabao ninao, mashabiki wasiwe na mashaka juu ya uwezo wangu.
“Nimeondoka Motema Pembe mimi mwenyewe bila ya kufukuzwa nikiwa nimeifungia timu yangu hiyo mabao 16, hivyo ninaamini nikiwa hapa nitaendelea na kasi yangu hiyo ya kufunga.
“Mimi nina uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, namba 7, 10 na 11, itategemea na kocha anataka anichezeshe nafasi gani kutokana na mfumo atakaoutumia na kuhusu miguu, ninatumia miguu yote miwili katika kufunga mabao na nikiwa Yanga ninatamani kuvaa jezi namba 3 (inayovaliwa na Ally Sonso),” alisema Morrison.
Aidha tulifanya mazungumzo na Nugaz kuzungumzia ujio wa Morrison alisema: “Kama unavyoona ndiyo nimekuja kumpokea hapa uwanja wa ndege na moja kwa moja ninampeleka kambini tayari kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Azam, suala la kucheza au kutocheza tunamuachia kocha.”
0 Comments