MOLINGA "FALCAO" ANAZIDI KUWA MTAMU, ATUPIA TENA KIGOMA

Klabu imekamilisha mechi zake za kirafiki katika ziara yake ya mkoani Kigoma kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kigoma United uliofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini hapa.


Ushindi wa huo umetokana na mabao ya mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), David Molinga Ndama ‘Falcao’ mawili dakika ya 22 na 88, wakati lingine limefungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 80.


Katika mchezo huo  wachezaji wawili wa Yanga walitolewa kwa kadi nyekundu kipa Ramadhani Kabwili dakika ya 81 na beki Cleophas Sospeter dakika ya 56 na kiungo anayetumika kama beki wakati mwingine, Jaffar Mohammed akaenda kusimama langoni kumalizia dakika 10.


Yanga SC ilikuwa wamenyane na wapinzani wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Mbao FC, lakini imeripotiwa timu ya Mwanza iligomea mchezo dakika za mwishoni kutokana na kutofikia makubaliano na waandaaji wa mchezo huo.

Na huu ulikuwa mchezo wa pili katika ziara ya Yanga mkoani Kigoma baada ya Ijumaa kuifunga timu ya Mwamgongo 2-1 katika mchezo wa kwanza.


Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo kuendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Iringa United mwishoni mwa wiki ijayo mjini Dar es Salaam. 


Kikosi cha Yanga SC  kilikuwa; Ramadhan Kabwili, Vincent Paschal/Paulo Godfrey ‘Boxer’dk80, Muharami Issa ‘Marcelo’, Cleophas Sospeter, Mustafa Suleiman, Ally Mtoni ‘Sonso’, Said Mussa/Mrisho Ngassa dk65, Said Juma ‘Makapu’, Gustaha Simon, Raphael Daudi na Jafari Mohammed.

Post a Comment

0 Comments