Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na aliyekuwa Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini.
Malinzi ametakiwa kulipa faini ya Shilingi 500,000 na Mwesigwa Shilingi milioni moja. Wote wamekubali kulipa kiasi hicho cha fedha.
Mahakama hiyo imetoa hukumu hiyo leo Jumatano baada ya kuwatia hatiani .
Wakati Malinzi akitiwa hatiani kwa shtaka moja la kutengeneza nyaraka za uongo, Mwesigwa alitiwa hatiani kwa kutumia nyaraka hizo.
Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wawili katika kesi hiyo ambao ni aliyekuwa mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Frola Rauya ambaye alikuwa karani.
Katika shtaka hilo Malinzi anadaiwa kutengeneza nyaraka hizo zinazoeleza kuhusu kikao cha kamati tendaji ya TFF kwa kubadili watia saini badala ya Edagar Masoud aliwekwa Mwanga.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha ambazo ni Dola 173,335 za Marekani.
0 Comments