Klabu ya Simba imeendelea kukaa kimya kuhusu suala la Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems na kuna uwezekano mkubwa akaondoka ndani ya klabu hiyo siku zijazo .
Kocha huyo hivi karibuni aliondoka nchini ghafla huku akiomba ruhusa kwa mabosi wake ikiwa ni saa chache kabla ya kusafiri ikielezwa kwenda kufanya mazungumzo na klabu ya Polokwane FC ya nchini Afrika Kusini atakayokwenda kuifundisha.
Wakati kocha huyo akiwa nchini humo taarifa zilienea lakini Simba tayari walikuwa wakifanya mazungumzo na Kocha wao wa zamani, Mserbia Goran Kopunovic.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo amospoti imezipata kocha huyo juzi usiku alikutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa na kufanya kikao kizito ambacho kilifikia muafaka mzuri wa pande zote mbili katika kusitisha mkataba.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa katika kikao hicho wamefikiana makubaliano ya kumalizia mchezo wa mwisho wa ligi kabla ya kusimama unaotarajiwa kupigwa lhapo jana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na Simba kuifunga Ruvu Shooting mabao 3-0.
Aliongeza kuwa ilitakiwa kocha huyo atangazwe tangu juzi lakini mchezo wa Ruvu ndiyo umevuruga mipango hiyo na walifikia kuchukua maamuzi hayo kwa kuhofia kuwavuruga kisaikolojia wachezaji watakapokuwa uwanjani.
“Ilikuwa ni ngumu kutangaza kuachana na kocha juzi Jumatano wakati tukiwa tunajiandaa na mchezo mgumu dhidi ya Ruvu, lakini ukweli ni kwamba mchezo wetu wa ligi wa kesho (jana) utakuwa wa mwisho kwake kukaa benchi yeye pamoja na benchi zima la ufundi.
“Kikubwa viongozi walikuwa wanahofia kutangaza kuachana na yeye kwa sababu ya kuwachanganya kisaikolojia wachezaji wetu tukielekea katika mchezo huo, hivyo kama viongozi wameona umuhimu wa mchezo huo kwa kumpa mechi ya mwisho yeye pamoja na benchi la ufundi kukaa kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja benchi.
“Hayo yote yalifikiwa muafaka baada ya kikao kizito kilichofanyika juzi usiku kati ya kocha huyo na mtendaji wetu mpya, hivyo Aussems atautumia mchezo kama sehemu ya kuwaaga wachezaji na mashabiki wa timu hiyo atakapokaa benchi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Aussems alizungumzia hilo mara baada ya mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja Gymkhana jijini Dar es Salaam na kusema kuwa: “Niwaondoe hofu mashabiki kuwa mimi bado kocha wa Simba na waachane na tetesi hizo zinazoendelea za mimi kufukuzwa, kikubwa wao wajitokeza uwanjani kuisapoti timu yao itakapokuwa ikicheza na Ruvu.”
Naye mtendaji wa timu hiyo, Senzo alisema kuwa: “Aussems bado kocha wa Simba, hizo taarifa siyo rasmi za kuachana na kocha wetu na nisingependa kuzungumzia hilo, hivi sasa akili zetu zote tumezielekeza kwenye mchezo wetu wa ligi dhidi ya Ruvu.”
Katika hatua nyingine,amospoti imepata taarifa za Bodi ya Utendaji ya timu hiyo kupitia baadhi ya makocha wanaotarajiwa kumrithi Aussems anayetarajiwa kuondoka wakati wowote nchini ikielezwa kuelekea Polokwane.
Habari za ndani zinadai kwamba Aussems ameshamalizana na Polokwane na anatakiwa kuwa kwenye benchi Jumanne dhidi ya Orlando Pirates kwani tayari aliyekuwa Kocha Mkuu ameshapigwa chini.
Kwa mujibu wa Gazeti la Soccer Laduma la Afrika Kusini, mechi dhidi ya Orlando ni ngumu kwa Polokwane na wanataka benchi pawe na Kocha mpya.
0 Comments