Timu ya Simba SC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa kirafiki usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
Bao pekee la mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo limefungwa na mshambuliaji wake mpya, Mbrazil Wilker Henrique da Silva kwa shuti kali dakika ya tano akimalizia pasi ya kiungo Mkenya Francis Kahata.
Simba SC leo iliongozwa na Kocha wake Msaidizi, mzalendo Dennis Kitambi kufuatia bosi wake, Mbelgiji Patrick Aussems kwenda kwao mara moja kwa kile kilichoelezwa 'sababu za matatizo ya kifamilia'.
Simba SC leo ilicheza vizuri mno tofauti na ilivyokuwa Jumamosi wakati wanafungwa 2-1 KMC ya Kinondoni katika mchezo mwingine wa kirafiki hapo hapo Azam Complex.
Mchezo wa leo kwa Simba SC ilikuwa ni maandalizi ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa JKT Tanzania mchezo wa leo yalikuwa maandalizi yao ya mwisho kabla ya kumenyana na Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu Ijumaa Uwanja wa Uhuru pia.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomary Kapombe, Kenedy Juma, Tairone Santos/Wawa dk46, Haruna Shamte, Gerson Fraga, Deo Kanda, Said Ndemla, Wilker Da Silva/Rashid Juma dk46, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata.
JKT Tanzania; Abdulrahman Mohamed, Anuary Kilemile, Adeyum Ahmed, Mohamed Fakhi, Rahim Juma, Mgandila Shaaban, Ally Bilal, Kelvin Nashon, Samuel Kamuntu, Hafidh Mussa na Najim Magulu.
0 Comments